Kwa Nini Si Lazima Tumsikilize Shetani

Sikiliza makala hii:

Ilikuwa ni mwanzo wa Januari. Wakati huo nilikuwa nimerudi nyumbani baada tu ya kufanya mazungumzo katika mikutano kadhaa. Siku hiyo nilimka huku nilikuwa nimekufa moyo, na kujihisi nimegandamizwa akilini. Nilikuwa na mawazo kama haya: “Maisha yangu yamekwisha. Tayari nishamaliza kuishi siku zangu za furaha. Huduma yangu imefika kikomo. Kamwe sijihisi kwamba Mungu ananipenda.” Ni kwa nini nikawa na mawazo kama hayo? Yalitoka wapi? Nilihitaji kufanya nini ili kuyaondoa akilini mwangu? Lakini siku hiyo ilipofika kikomo tayari nilikuwa najihisi vyema kabisa. Uchangamfu wangu ulikuwa umerudi na nikawa mtu mwenye tumaini. Lakini ni jambo gani nililolijua hapo mbeleni ambalo ndilo lilileta mabadiliko hayo akilini mwangu? Jambo hilo ndilo nataka kushiriki nawe, ili wewe pia uweze kuwa na ushindi wakati hofu na hisia za kufa moyo zimeingia ndani mwako, au wakati ambapo vita vya kiroho vimekufikia.

Kutokana na huduma yangu ya miaka mingi nimekuja kujua kwamba tunaye adui wa nafsi zetu. Kamwe hatuwezi kumwona, lakini kwa kweli yeye yupo. 1 Petro 5:8 inasema, “Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. Muwe imara katika imani na kumpinga.” Sisi humpinga adui huyu kwa kuwa imara wokovuni na pia kwa kuamini Neno lake Mungu.

Shetani ni Nani?

Lakini Shetani ni nani hasa? Ni yeye ambaye Maandiko huita “yule mwovu.” Yeye kamwe si kiumbe kilicho kinyume na Mungu kwa njia ya ukamilifu, kwa sababu Shetani hayuko katika hali moja na Mungu, kwani Mungu kamwe hana mwenza. Hakuna anayetoshana na Mungu. Kwa kweli Shetani ni malaika ambaye tayari ashahukumiwa na Mungu. Yeye anajaribu kuwa na nguvu juu ya Wakristo, lakini tunaambiwa kwamba sisi, “tuna nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu” (1 Yohana 4:4).

Lakini Shetani hujaribu kufanya Wakristo wafe moyo. Yeye huwa akitujaribu ili tutende dhambi na pia kutujaribu ili tusiweze kumwamini Mungu. Yeye ni mpinzani wetu. Kamwe hatumwoni, lakini yeye yuko. Yesu mwenyewe alituombea ili Baba atulinde kutoka kwa yule mwovu (Yohana 17:15).

Katika Maandiko Shetani anaitwa mshtaki, mkashifu, baba wa uongo, muuaji, mdanganyifu, adui. Mtume Paulo anatwambia katika Waefeso, “Maana vita vyetu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu, wanaomiliki ulimwengu huu wa giza” (Waefeso 6:12). Kuna kiumbe ambacho tunapigana nacho. Kwa kweli hatustahili kuwa watu ambao hawana ufahamu katika swala hili.

Lakini hakuna haja ya sisi kuogopa. Kamwe mimi siwezi kukuhimiza eti uwe makini kwa mambo ya giza, hata ingawa giza lenyewe lipo. Badala yake mimi ningetaka wewe kujua ule ushindi ambao tuko nao ndani yake Kristo . . . ukweli na usalama ambao ni wetu.

Je, Shetani hufanya kazi kwa njia gani? Yeye hufanya vipi? Kazi kuu ya Shetani ni kujaribu kutudanganya—kujaribu kufanya jambo kuonekana kuwa la kweli kumbe ni uongo mtupu; ni hadaa tupu. Dkt. Neil Anderson wa Huduma ya Uhuru Katika Kristo (Freedom in Christ Ministries) amesema mambo kadhaa muhimu.

Biblia imenena kuhusu Shetani kwa njia tatu:

  • mshawishi (Mathayo 4:3)
  • anayewashtaki ndugu Wakristo (Ufunuo 12:10)
  • baba wa uongo (Yohana 8:44)

Ndiposa Dkt. Anderson akasema, “Kama nikikushawishi jambo fulani, bado wewe utajua kwamba ninakushawishi. Nikikushtaki, wewe utajua kwamba nakushtaki. Lakini mimi nikikuhadaa, kamwe huwezi kujua kwamba ninakuhadaa. Nguvu za Shetani zipo katika uwongo wake. Ukijua uongo wake utamnyang’anya nguvu zake.”

Kumkabili Shetani

Sisi tunaweza kuukabili uwongo wa Shetani kwa njia gani? Kwa kuzingatia yale ambayo Mungu amesema. Kwa mfano, kama ukijisikia kwamba wewe ni Mkristo ambaye hafai, pengine kwa sababu hujautumia muda wako mwingi katika maombi au katika kusoma Neno lake Mungu, ndiposa sasa unahisi kwamba umemkosea Mungu kwa njia fulani na ukaanza kufikiri, “Kwa kweli Mungu amenikasirikia, naona atanitupilia mbali.” Lakini Neno lake Mungu linasema nini? “Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6). Na pia, “Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo” (Warumi 8:1).

Au pengine unafikiria, “Kwa kweli Mungu kamwe hanipendi. Kama angalinipenda mimi singekuwa na shida hizi zote.” Huenda unajihisi kwamba huo ndio ukweli wa mambo, lakini Neno la Mungu linasema nini? Yesu akasema, “Mimi nimewapenda nyinyi kama vile Baba alivyonipenda mimi” (Yohana 15:9). “Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda . . .” (1 Yohana 4:10). “Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu” (1 Yohana 3:1).

Au tuseme kwamba sababu ya wewe kufa moyo ni dhambi fulani ambayo umetenda na ambayo Shetani anaitumia kukuhukumu, huku akikwambia kwamba kamwe Mungu hatakusamehe dhambi hiyo. Huo ni uwongo. Ni kwa nini tunasema hivyo? Neno la Mungu linasema nini? “Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote” (1 Yohana 1:9).

Hebu tutoe mfano mwingine. Pengine umeanza kuvutiwa na mtu fulani kimapenzi, halafu yeye anaanza kukwambia, “Tukifanya tendo la ngono jambo hilo halitamkasirisha Mungu, kwa sababu sisi tunapendana sana.” Lakini Neno la Mungu linasema nini? “Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu . . .” (Waebrania 13:4). “Mungu anataka nyinyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu” (1 Wathesalonike 4:3-5).

Kamwe hatustahili kuruhusu hisia zetu, mawazo yetu, au uwongo wa Shetani kutwambia ni jambo gani lililo la kweli. Neno la Mungu ni la kweli kushinda hisia zetu zote, mawazo yetu yote, na mambo yote ambayo twayaona kwa macho yetu. Shetani huwa akijaribu kutuchanganya akilini mwetu, lengo lake likiwa kufanya tufikirie kwamba kuna kitu ambacho Mungu anatunyima. Lakini Mungu ndiye ambaye alituumba na kutupenda sana, hivi kwamba akafa kwa ajili yetu. Katika kumkabili Shetani hauna budi kujua ukweli.

Unahitaji kujua Neno lake Mungu ili liweze kukuweka huru. Tumeambiwa kwamba tumpinge Ibilisi huku tukiwa “Imara katika imani” (1 Petro 5:9). Imani si hisia. Ni uamuzi ambao sisi hufanya wa kuchukua Neno la Mungu kuwa la kweli. Ili tupate uhuru katika vita vya kiroho tunahitaji kuchukua mawazo yetu, hisia zetu, na majaribu yetu na kujiuliza swali lifuatalo, “Je, Neno la Mungu linasema nini kuhusu jambo hili?” Katika Yohana 17, punde tu wakati Yesu alipomaliza kufanya maombi kwa Baba yake, “uwakinge na yule Mwovu,” wajua ni jambo gani alisema baada ya hayo? akasema, “Waweke wakfu katika ukweli; neno lako ni ukweli” (Yohana 17:17). Na pia Yesu akasema, “Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru” (Yohana 8:32).

Mimi nimegundua kwamba ni jambo muhimu sisi kujua kitambulisho (chetu) ndani yake Kristo. Katika kitabu cha Waefeso mtume Paulo anaandika na kusema, “Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua . . . jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini,” kwetu sisi ambao tunachukulia Neno lake kuwa ni la kweli (Waefeso 1:18-19). Mungu anaishi ndani yetu na kutupatia nguvu.

Basi tunapojipata kwamba tuna mawazo yasiyofaa ku(ji)husu sisi wenyewe, au kuhusu Mungu, au pia watu wale wengine, tunahitaji kufanya nini na mawazo kama hayo? Waefeso 6:16 inasema, “imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.” Andiko hili linasema tutaweza kuzima mishale YOTE ya yule Mwovu. Haya ni mawazo ambayo yanaweza kutujia na kumbe hata hatujui yametoka wapi—yanatujia kama mishale ya moto. Tutafanya nini basi? Tazama andiko hilo linasema kwambwa “tukiwa na ngao ya imani.” Hili ndilo jambo ambalo ni lazima sisi kufanya. Katika vita vya kiroho hatuwezi kukaa na kutofanya lolote. Yakobo 4:7 inasema, “Mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni.” Ni lazima tufanye uamuzi wa kuchukulia Neno la Mungu kuwa la kweli. Kama unashambuliwa kwa mshale wa moto, lengo la mshale huo huwa ni mawazo yako.

Je, ushawahi kufikiria kwamba ILIKUWA LAZIMA wewe kuanguka dhambini baada ya kupata majaribu, kama kwamba Shetani anajaribu kukuonyesha kwamba kamwe huwezi kupigana na jaribu la aina hiyo? Kuna andiko ambalo tunafaa kukariri, ili tuweze kuliweka akilini mwetu na kuweza kulikumbuka wakati wa majaribu: “Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.” (1 Wakorintho 10:13).

Kuteka Fikira Zote

Shetani kamwe hawezi kusoma mawazo yetu, lakini yeye anaweza kupanda fikira katika mawazo yetu. 2 Wakorintho 10:5 inasema, “. . . tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo.” Lakini ni fikira za aina gani ambazo tunahitaji kuziteka? NI fikira ambazo huja akilini mwetu ambazo ziko kinyume na kile ambacho Mungu amesema. Mawazo ambayo huja akilini mwetu ambayo ni kinyume cha yale ambayo Mungu amesema kuhusu Yeye binafsi, au kuhusu watu wale wengine.

Mawazo ndiyo ambayo huzua matendo; nayo matendo huzua tabia. Na chanzo cha haya yote ni fikira. Mungu anataka tuamini Neno lake zaidi ya jinsi ambavyo tunaamini hisia zetu, zaidi ya vile ambavyo mambo yanaonekana machoni mwetu. Neno la Mungu ni la kweli zaidi ya mambo yote ambayo twaweza kufikiria. Ni la kweli zaidi ya hisia zangu zote. Ni la kweli zaidi ya jinsi mambo yanavyo-onekana. Biblia inasema, “Majani hunyauka na ua hufifia, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele” (Isaya 40:8). Katika Zaburi Daudi anasema, “Neno lako ni . . . mwanga katika njia yangu” (Zaburi 119:105).

Yesu alitoa mfano ufuatao huku akisisitiza umuhimu wa sisi kusikia na kutenda kulingana na Neno lake . . . “Kwa hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba” (Mathayo 7:24,25). Na akaendelea kusema, “Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike” (Yohana 15:10,11).

Tunaweza kusimama wima dhidi ya hali yoyote ile, mawazo au hisia zozote zile, kwa kutazama Mwamba wetu (Zaburi 18:46), Yeye ambaye anatupenda na kutuongoza kwa ukweli wote (Yohana 16:13). Shetani anaweza kutujaribu, kutufanya tufe moyo, kutushinda. Lakini yeye ni mwongo, na tunahitaji kukabiliana na uongo wake kwa ukweli wa Neno lake Mungu. Basi tunapofanyisha kazi ngao ya imani yetu kwa Neno la Mungu, tutakuwa washindi ndani yake Kristo.

“Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu, anayeipa
mikono yangu mazoezi ya vita, na kuvifunza vidole vyangu kupigana.
Yeye ni rafiki yangu amini na ngome yangu,
kinga yangu na mkombozi wangu;
yeye ni ngao yangu, kwake napata usalama; . . .”
Zaburi 144:1,2

“Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,
sote pamoja tulisifu jina lake.
Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,
na kuniondoa katika hofu zangu zote.
Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.
Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.
Mateso ya mwadilifu ni mengi,
lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.”
Zaburi 34:1,3,4,8,19

“Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu,
kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu.
Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi,
na uaminifu wako nyakati za usiku.”
Zaburi 92:1,2