Je, Mungu Yupo Maishani Mwangu Sasa?

Sikiliza makala hii:

Wakati ulifanya uamuzi na kumwalika Yesu kuingia maishani mwake, ni muhimu sasa wewe kujua kama kwamba Mungu alikusikia. Yesu alituahidi kwamba ataingia maishani mwetu mradi tu tukimwomba kufanya hivyo.

Katika Ufunuo 3:20 Yesu ametuahidi, “Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami.” Je, wewe ulimfungulia Mungu kuingia moyo wako? Kama ulifanya hivyo Yeye ameahidi atafanya nini? Je, Mungu anaweza kutudanganya?

Yohana wa Kwanza 5:14 inasema kwamba, “Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza.”

Na katika Yohana 6:37 Yesu alisema, “Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu.” Na katika Yohana 10:27-29 Yesu anasema, “Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.”

Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, ili kwamba tuwe na uhusiano na Yeye. Na Yeye anajali sana kuhusu swala hili. Yesu alifanya yote yaliyohitajika ili kutuleta katika uhusiano pamoja naye. Yeye alichukua dhambi zetu na akatuvalisha utakatifu wake, na kufanya tusamehewe dhambi kabisa na kukubaliwa naye kabisa. Hatuna haja ya eti kwanza kuishi maisha mazuri, au kufanya sherehe za kidini, au kutumia miaka mingi tukimwomba kabla ya kumpokea. Mungu mwenyewe ndiye alifanya iwezekane kwamba tuwe na uhusiano naye. Na sisi tunaenda kwake kutokana na kile ambacho Yeye alitufanyia, sio kile ambacho tunaweza mfanyia. Yeye alilipia dhambi zetu, ili kwamba atusamehe na kuingia maishani mwetu. Waraka wa Kwanza wa Petro 3:18 inasema, “Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu.”

Wakati mtu amemwomba Yesu kuingia maishani mwake, ni jambo la furaha akijua mambo ambayo Mungu amesema ni kweli kuhusiana na uhusiano wake na Mungu.

 • Sasa wewe uko na uhusiano wa amani na Mungu – “Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.” (Warumi 5:1)

 • Unafanyika mtoto wa Mungu – “Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.” (Yohana 1:12)

 • Sasa wewe huishi gizani tena – “Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga.” (Waefeso 5:8)

  “Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.” (Wakolosai 1:13,14)

 • Umesamehewa – “Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake.” (Matendo 10:43)

  “Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo!” (Waefeso 1:7,8)

  “Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu.” (1 Yohana 4:9,10)

 • Umepewa uhai wa milele – “Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uhai.” (Yohana 5:24)

  “Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uhai wa milele, na uhai huo uko kwa Bwana. Yeyote aliye na Mwana wa Mungu anao uhai huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana uhai. Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uhai wa milele nyinyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu.” (1 Yohana 5:11-13)

 • Umewekwa muhuri wa Roho Mtakatifu – “Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia.” (Waefeso 1:13)

 • Waweza kuanza kujua upendo wa Mungu kwako – “Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. Mimi nimewapenda nyinyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.” (Johana 15:7-11)

Ili uweze kukua katika uhusiano wako na Mungu:

Ili kumjua Mungu vizuri zaidi tumia wakati wako kusoma Neno lake (Biblia) na kumwomba ajidhihirishe zaidi kwako na ajenge uhusiano kati yako na Yeye. Injili ya Yohana (kitabu cha nne katika Agano Jipya) ni mahali panapofaa kuanza kusoma Biblia.

Ongea na Mungu kwa njia ya uwazi. Yeye anatuhimiza, “Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.” (Wafilipi 4:6,7)