Roho Mtakatifu Akiwa Ndani Yetu

Sikiliza makala hii:

Wengine wetu hufikiria, “Kama Yesu angalikuwa hapa duniani na tuweze kumwona kwa macho sisi tungemfuata kila mahali.” Lakini Bwana anasema katika Ezekieli 36:27 “Nitatia Roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu.” Kuna jambo tunahitaji kuzingatia kuhusiana na maneno yaliyotumika katika mstari huu, neno “ndani.” “Nitatia Roho yangu ndani yenu.” Kuna wakati ambapo nilihitaji kukumbushwa kwamba Roho wa Mungu yuko ndani yangu. Nakumbuka nikisoma maneno hayo na kwa siku nyingi nilitembea huku na huko nikifikiria, “Roho wake yumo ndani yangu!” Kristo yuko ndani mwangu kwa njia ya Roho wake hata leo, kama ambavyo alikuwa na wanafunzi wake. Ni jambo la ajabu mtu kutambua kwamba Roho wa Kristo anaishi ndani yetu ilhali wakati mwingi kamwe hatumtilii Yeye maanani.

Mahali Ambapo Roho Mtakatifu Anaishi

Wakorintho wa Kwanza 3:16 inasema, “Je, hamjui kwamba nyinyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” Naye mwandishi Andrew Murray alifafanua swala hili katika kitabu chake The Spirit of Christ (Roho wa Kristo) kwa njia ambayo imenisaidia sana. Anasema kwamba katika hekalu ya Wayahudi kulikuwa na ua tatu: ua wa nje, ua wa ndani, na Patakatifu pa patakatifu.

Mwandishi Murray alieleza kuhusu miili yetu kama ua wa nje. Nao ua wa ndani ni akili zetu, nia zetu, na hisia zetu. Lakini ndani mwetu kuna Patakatifu pa patakatifu ambako ndiko Roho wa Mungu hudumu. Roho Mtakatifu hudumu ndani ya roho zetu. Basi ndani mwako na ndani mwangu mna Patakatifu pa patakatifu. Patakatifu pa patakatifu pako ndani mwetu. Mstari wa 17 wa sura hiyo unasema, “Hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni nyinyi wenyewe.” Jambo hilo litakusaidia kujifikiria vizuri kwa kutambua kwamba mahali Patakatifu pa patakatifu pako ndani yako na ndani yangu.

Basi sisi tutadumisha hekalu letu likiwa safi kwa njia gani? Tunapomkubali Kristo damu yake hututakasa. Kwa hivyo tutaweza kuidumisha hekalu yetu katika hali ya kutakaswa kwa njia ya imani. Kwa kuchukua Neno la Mungu kuwa la kweli.

1 Yohana 1:9 ni mstari ambao mimi napenda kuita “sabuni ya kumwosha Mkristo.” Mstari huo wasema hivi, “Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote.”

Je, mara ya mwisho wakati wewe ulinawa mikono wakati ambapo mikono hiyo ilikuwa michafu sana wewe ulisimama hapo katika sinki na kutazama mahali ambapo maji machafu yalimwagika na kujiuliza swali, “Na huo uchafu wote wangu umeenda wapi, mimi ninasumbuka sana kwa ajili ya jambo hilo?” La hasha. Kwa imani wewe ulikubali kwamba maji hayo yaliingia katika mfereji wa maji taka. Hukuwaza kuhusu uchafu huo hata kidogo. Hivyo ndivyo tunahitaji kufanya. Tunapokiri dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu; na Yeye ni mwenye haki kutusamehe dhambi zetu na kututakasa kutokana na uovu wote. Tunahitaji kuamini kwamba Yeye ametusamehe hata ikiwa hatuoni au kuhisi hivyo.

Kila wakati Roho Mtakatifu hutuelekeza kwa Kristo. Yeye kila mara anatuelekeza mahali kuliko na msamaha, kwenye msalaba, na kwenye damu ya Kristo. Yeye daima anatuelekeza katika mahali ambapo hamna hukumu. Kwa nini? Kwa sababu Warumi 8:1 inasema, “Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo.”

Lakini Shetani naye hufanya nini? Yeye anataka kukunyang’anya amani ambayo Mungu amesema ni yetu. Yeye hujaribu kukurudisha nyuma ili uwaze kuhusu dhambi yako ambayo unaona ni mbaya sana. Basi hapo ndipo unawaza kuhusu mambo hayo, na yanakuwa kama video akilini mwako. Lakini tunachohitaji kufanya ni kuleta dhambi hizo chini ya msalaba na kusema, “Bwana Yesu, jambo hili ni ushahidi kwamba mimi ninahitaji Mwokozi. Bwana, asante kwa sababu ya damu ya Yesu Kristo ambayo hunitakasa kutoka kwa dhambi zote.” Hebu waza kuhusu dhambi zako kupitia kwa macho yanayotazama msalaba na kupitia kwa damu yake Kristo, na hapo utapata amani yake Mungu. Usifanye kukumbuka dhambi za kale. Amini msamaha wake Mungu.

Roho Mtakatifu Anasema Nasi

Tuseme nini kuhusu dhambi zetu za sasa, dhambi ambazo pengine Mungu anakuonyesha?

Njia ambayo Mungu hutumia kwangu mimi kuliko njia ingine yoyote ile ni kupitia kwa mahusiano yangu na watu wale wengine. Wakati mmoja nilikuwa na uhusiano fulani ambao ulinisumbua kwa miaka mingi. Nilikuwa na wakati mgumu sana na mtu huyo hata nikafikiria, “Kama wewe utaenda mbinguni mimi hata sitaki kufika huko.” Nilikuwa ninamnyoshea mtu huyo kidole cha lawama. Nilikuwa namlaumu sana. Nilikuwa ninamhukumu. Nilikuwa namwonea makosa. Nilikuwa sina jambo njema la kusema kuhusu mtu huyo. Na wakati huo wote mimi nilikuwa najiondolea lawama.

Lakini siku moja Bwana alinielekeza kwa Luka 18:9, “Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.” Nikatambua kwamba kwa kweli mimi nilikuwa namwonyesha mtu huyu madharau. Huu ndio mfano ambao Yesu alitoa:

“Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtozaushuru. Huyo Mfarisayo (aliyejiona mwenye haki ya kibinafsi, mwenye kiburi, kiongozi wa kidini katika wakati wa Yesu) akasimama, akasali kimoyomoyo: ‘Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtozaushuru (mla hongo, mwenye kuwekea watu wale wengine mizigo mikubwa ya ushuru, ambaye amechukiwa sana). Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.’ Lakini yule mtozaushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: ‘Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.’ ”

Yesu akatoa maelezo kwa mfano huo, “Nawaambieni, huyu mtozaushuru (aliyesema, Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi) alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.”

Niliposoma hayo nilijipata nikisema, “Bwana wangu, mimi sasa ni kama Mfarisayo huyo. Nachukia sana hivi nilivyo sasa. Ninamtazama mtu huyu kwa madharau.” Nikatambua kwamba nilihitaji kutazama moyo wangu mwenyewe. Nilipoanza kujitazama moyoni mwangu nikapata ndani mwangu mlijaa wivu, kukosa upendo, kiburi, hasira, kuwahukumu watu wengine, kuwanyoshea kidole. Ndipo hapo nikatazama Wagalatia 5:16-23, “Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia . . . Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi; kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano; husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo.”

Wakati mwingi sisi tunatazama orodha ya dhambi na kujiambia, “Kwa kweli mimi sijipati humo.” Lakini wajua kile ambacho sisi hukosa kufanya? Tunakosa kujitazama na kujipima kwa orodha ya tunda la Roho na kusema hivi, “Je, kipimo changu cha upendo ni kipi? Na kipimo cha fadhili zangu? Je, uaminifu wangu uko na kipimo kipi? Na upole wangu wapimaje?” Kwa kweli wakati mwingi sisi hujipima kwa njia ya vipimo vya dhambi zetu badala ya kujipima kwa tunda la Roho.

Mwandishi Andrew Murray alisema, “Ni kwa nini sisi huwa tunakutana na Wakristo ambao ni watakatifu mno lakini pia ni wakali mno?” Akaendelea kusema, “Ni kwa sababu wao hawajui lolote kuhusu Roho wa upendo. Roho Mtakatifu ndiye pekee anayeweza kuzaa upendo.”

Nilipoendelea kufikiria kuhusu mtu yule ambaye alinifanyia makosa nilikumbushwa kuhusu 1 Petro 3:8,9: “Mwisho nasema hivi: mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka.”

Kwa kweli nilijihisi kwamba mtu huyo alikuwa amenifanyia mambo maovu, alikuwa amenifanyia matusi. Lakini Maandiko yalisema “Msiwalipe watu ovu kwa ovu” badala yake, “watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka.”

Nilipotambua kile ambacho kilikuwa moyoni mwangu na kukiri kwamba mimi nilikuwa kama Mfarisayo hapo ndipo niliomba, “Bwana, unisamehe kwa maana mimi ni mwenye dhambi. Bwana, naomba unionyeshe jinsi ya kupatia mtu huyu baraka.” Wakati huo nilikuwa hapo Uingereza, na katika moja ya maduka ya vitabu humo nilikumbuka kuona kitabu kimoja ambacho kilikuwa cha bei ghali, lakini ambacho nilijua kwamba kwa hakika mtu huyo angekipenda. Basi niliporudi Marekani mimi nilimpatia mtu huyo kitabu hicho. Hebu nikwambie, yeye aliguzwa sana na tendo hilo langu. Aliona kwamba hiyo ndiyo zawadi kubwa zaidi ambayo mtu angeweza kumpatia, na mimi nikaona kwamba Mungu alitumia kitabu hicho kwa njia kubwa sana.

Daima Roho Mtakatifu atakuwa mwaminifu kutuonyesha mahali ambapo hatuwi kama Kristo. Yeye alikuwa mwaminifu kunionyesha mahali ambako sikuwa kama Kristo. Tunaposoma Neno la Mungu na kumwomba Roho Mtakatifu kutuongoza kwa njia ambazo zinampendeza, Yeye atakuza tunda la Roho ndani mwetu: “upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.”

Yesu akasema, “Mimi nimewapenda nyinyi kama vile Baba alivyonipenda mimi . . . Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike” (Yohana 15:9,11).

Makala haya yamenukulia kwa kibali kutoka kwa kitabu Faith Is Not a Feeling (Imani Hailingani na Hisia Zako), kitabu cha Ney Baile.