Vile Ambavyo Mungu Hutubadilisha

Sikiliza makala hii:

Mara nyingi sisi hujipata kwamba kuna sehemu zingine maishani mwetu ambazo zingali zinatusumbua; sehemu ambazo tungetaka ziwe tofauti. Pengine ni ukosefu wa uadilifu sehemu fulani ya maisha yetu, au ni tabia mbaya ambayo ingali inatutawala na kufanya tufe moyo. Je, Mungu anataka tufanya nini kuhusu maswala kama haya? Je, kuna njia ya sisi kuweza kupata uhuru na mabadiliko ya kweli? Ndio. Ukweli ambao sasa mimi najua kuhusu neema yake Mungu umeleta mabadiliko makubwa maishani mwangu. Na mimi naamini kwamba ukweli huo unaweza kuleta tofauti kubwa maishani mwako.

Unaposikia neno neema, ni mawazo gani yanakuingia akilini? Naonelea kwamba maana bora zaidi ambayo imetolewa kwa neno hilo ni ile ya mwandishi Joseph Cooke, ambaye aliandika na kusema, “Neema sio kitu kingine ila ni uso ambao upendo unavaa unapokutana na hali ya mwanadamu kukosa ukamilifu, kuwa na udhaifu, kuwa ametenda makosa, au ametenda dhambi.”

Neema ni nini?

Ni sifa ile iliyoko moyoni mwa Mungu ambayo humwezesha kutushughulikia kwa njia ambayo hailingani na dhambi zetu, au anakosa kujilipiza kisasi dhidi yetu kulingana na vile ambavyo dhambi zetu zinastahili. Neema ni uaminifu wa Mungu kwetu, hata wakati ambapo hatuwi waaminifu. Kwa kweli neema ni kile ambacho upendo huwa, wakati umekutana na kitu ambacho hakipendeki, chenye udhaifu, kisicho kamili, na kisicho stahili, na hata cha kudharauriwa. Mungu ana uwezo wa kushughulikia mahitaji yetu bila kuzingatia kustahili kwetu. Hizi ni fadhili ambazo mtu hupata bila kustahili.

Neema ya Mungu huleta upendo, fadhili, na kupendelewa kwa wale wote wanaomtumaini Yeye. Hakuna haja ya mtu kulipa gharama. Kile unahitaji tu ni kuwa na uhusiano na Yeye ili upate neema yake.

Wakati ule ambao tunahitaji sana neema ya Mungu ni wakati tumetambua kwamba kuna sehemu fulani maishani mwetu ambayo tumeenda mrama—vitendo kama vile: kufanya maamuzi mabaya, kuwa na tabia mbaya, kufanya mambo ambayo tunayaonea aibu; kutambua sehemu fulani maishani mwetu ambayo tungetaka Mungu kutubadilisha, lakini badala yake sisi tunajihisi kwamba hukumu yake iko juu yetu. Kama tushampokea Kristo mioyoni mwetu, basi tayari tushatangazwa kuwa wake, tumesamehewa, na tunaishi kwa neema zake. Neema yake ndio hutuweka huru na kutubadilisha. Ndiposa ni muhimu kwetu kujua yale ambayo Maandiko yanasema kuhusu neema ya Mungu.

Twasimama Ndani ya Neema
(tazama Warumi 5:2)

Kusema kweli sisi hutambua kwamba ndani yetu kuna sehemu nzuri lakini pia kuna sehemu mbaya. Tuna sehemu ambayo tunataka ulimwengu kuona—sehemu ile ambayo tumesimama wima kitabia. Lakini pia tunayo sehemu ambayo tunataka kuficha, kwa sababu tunaionea aibu.

Sisi tunaishi katika utamaduni ambao watu hupenda kujiimarisha. Tunatumia wakati mwingi na bidii nyingi ili kijiboresha huku tukijaribu kujua jinsi ya kuimarisha sehemu zetu ambazo sio nzuri. Ndiposa tunaenda dukani kununua virembeshi, au kwenda kufanya mazoezi katika ukumbi wa kujenga misuli ya mwili, na kutumia bidii na pesa nyingi tukijaribu kuboresha sehemu hizo ambazo hazipendezi maishani mwetu. Lakini sehemu zile ambazo kamwe hatuwezi kuimarisha, au zile ambazo bado hatujafaulu kuimarisha, sehemu hizo tunazificha.

Kujificha Kutokana na Aibu

Je, ushajipata kwamba mmekutana na mtu ambaye mmeanza kujuana hivi karibuni na ndani mwako unaanza kusema, “Ni tumaini langu kwamba mtu huyu hatajua ukweli huu kuhusu maisha yangu?” Au ukamwambia rafiki yako wa karibu, “Tafadhali usimwambie mtu yeyote ukweli huu kuhusu maisha yangu.” Vivyo hivyo tunapoanza uhusiano wetu na Mungu tunaweza kufikiri kwamba Yeye yuko kama sisi. Tukafikiri kwamba tunahitaji kumficha sehemu zetu ambazo hazifai. Lakini tukijaribu kuficha sehemu kama hizo tunaweza kukosa ukweli kwetu sisi binafsi, au kukosa kuwa wakweli katika mahusiano yetu na Mungu.

Mungu wetu hayuko hivyo. Njia zake sio njia zetu. Yeye hakubali sehemu zetu ambazo ni nzuri, na kukataa sehemu zetu ambazo hazifai. Yeye anatuona kama watu kamili. Mungu hatuoni kama watu waliogawanyika vipande vipande. Yeye anasema, “Wewe usijaribu kufanya sehemu yako mbaya kuwa nzuri kwani ukiwa peke yako huwezi kufaulu katika jambo hilo. Haijalishi utaimarisha sehemu hiyo kwa kiwango kipi, kamwe hautafikia kiwango changu, kwa sababu mimi ni mkamilifu. Wewe nipe sehemu zako nzuri, na pia unipatia sehemu zako ambazo ni mbaya, na pia unipatie nafasi ya kukufanya uwe mtu mkamilifu.”

Tunawezaje kupata neema ya Mungu maishani mwetu?

Ni vigumu mtu kuelewa neema bila kufahamu sheria. Katika Biblia tunaona sheria kamili ya Mungu, amri zake, na jinsi ambavyo Yeye angetaka tuishi . . . na kwa kweli sisi kamwe hatuwezi timiza hayo yote. Sasa tufanyeje kwa sababu ya sheria na amri za Mungu? Sheria ni kama kioo kwetu. Unapotazama kioo unaweza kutambua kwamba ulikuwa na uchafu mwingi usoni mwako, ambao mbeleni hukujua kwamba upo. Lakini kioo hakiwezi kukuondolea uchafu huo, lakini ungali unakuwa na shukrani kwa sababu ya kutazama kioo kabla ya kutoka nyumbani kwenda shughuli zako. Vivyo hivyo sheria yake Mungu hutuonyesha upungufu wetu, dhambi zetu, na tunakuwa na furaha kubwa kwa kuweza kuona hayo yote, ili tuwe na nafasi ya kuleta yote kwa Mungu, ili Mungu naye atushughulikie kwa njia ya neema yake. Wagalatia 3:24 inasema, “Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu.” Tunapokuja kwa Kristo tunatambua kwamba tunahitaji Mwokozi. Ukweli ni kwamba, katika maisha yetu yote ya baadaye, daima tutahitaji mwokozi.

Nayo Waebrania 4:13-16 inasema: “Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake yeye ambaye kwake tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu. Basi, tuzingatie kwa makini imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka mbinguni; Yesu, Mwana wa Mungu. Huyu Kuhani Mkuu wetu anaelewa kabisa unyonge wetu; yeye mwenyewe alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.”

Enda Kwake kwa Ukweli na Unyenyekevu

Tunaweza kupata neema maishani mwetu wakati tumekuja kwa kiti cha neema kwa ukweli na unyenyekevu. Kinyume cha kufika hapo kwa ukweli, ni wakati ambapo tunajaribu kujificha na kukosa kuleta mambo yetu katika mwanga.

Hapa nitafungua moyo wangu peupe na kushiriki nanyi sehemu maishani mwangu ambayo nilihitaji kuleta kwa Bwana, kuileta kwa kiti chake cha neema. Kwa muda mrefu maishani mwangu swala la chakula limekuwa shida kubwa. Kwa kweli sikumbuki nikiwa mtoto mnene hapo utotoni wangu, lakini ninakumbuka nikiwa kidato cha tatu marafiki zangu (ambao walikuwa na uzito mdogo kunishinda) wakinugunika kwa sababu ya wao kuwa wanene. Ndiposa nami nikafikiria, “Kama hawa wanadhani kwamba ni wanene, na mimi nina ratili nyingi kuwashindi, si hii ni kumaanisha kwamba mimi ni mnene zaidi!” Wakati huo mimi nilikuwa na uzito wa ratili 118. Ninakumbuka ni wakati huo ndipo chakula kilianza kuwa shida maishani mwangu. Na nikaanza kufikiri kuhusu kile ambacho mimi sistahili kula ili nisinenepe zaidi, jambo ambalo liliniletea shauku zaidi ya kutaka kula.

Mamangu mzazi naye angesema maneno kama yafuatayo, “Naonelea wewe utakuwa wa kupendeza zaidi wakati ukivaa nguo zako ikiwa hautakula chakula cha aina hii. Na ni kwa nini wewe hupunguzi uzito wako?” Hata ikafika mahali pa yeye kunipeleka kwa daktari wa kupunguza uzito.

Halafu wakati nilienda chuo kikuu, huku nikijua kwamba kuna chakula cha aina fulani ambacho sikustahili kula, mimi kwa kweli nilikuwa nanunua chakula hicho na kukificha. Ikafika wakati ambapo hata nilificha chokoleti katika kabati yangu ya nguo. Na wakati moja nilificha keki ya uzito wa ratili kumi mvunguni wa kitanda changu. Na kama mtu angeniambia kwamba sistahili kula chakula cha aina fulani, jambo hilo lilinipatia shauku zaidi ya kula chakula cha aina hiyo mara kumi zaidi. Humo katika chuo kikuu kulikuwa na duka mbili za kununua hambaga. Ninakumbuka nikienda kwa duka moja na kusema nipewe hambaga moja iliyowekwa jibini, ikiwa pamoja na chipsi na chupa ya soda ya kokakola, na nikala mara moja. Halafu nikaenda kwa gari langu na kwenda kwa duka lingine la hambaga, na kusema nipewa hambaga nyingine ya jibini, chipsi na maziwa tamu – na nikala hizo pia papo hapo. Na kama niliona aibu kuitisha vyakula hivyo mahali pamoja, ningeenda mahali pa pili. Lakini kama singekuwa na muda mwingi, ningeenda mahali hapo pamoja na kusema, “Saasa, naona nataka hambaga ya jibini, chipsi, na soda ya kokakola.” Tena ningeongezea na kusema, “Ha! Huyu jirani yangu alitaka nini? Aa--nimekumbuka, yeye pia anataka hambaga ikiwa na soda ya kokakola na chipsi.” Basi ningejifanya kama kwamba nilikuwa nanunua chakula cha watu wawili. Na ningetoka mahali hapo na kula chakula hicho chote. Lakini nikiwa kama nimejificha. Na kusema uongo.

Uhuru wa Kutokuwa na Haja ya Kujificha

Nilipokuja kwa Kristo, Yeye alinikubali, na pole pole kwa jinsi ambavyo miaka ilisonga mbele niliweza kupata kiwango fulani cha uponyaji kwa swala la shida ya chakula. Mbeleni nilikuwa mlaji ambaye hangeweza kamwe kujizuia, lakini miaka ilivyoendelea Bwana aliniondolea msukumo huo wa kutaka kula.

Lakini wakati mwingine mimi huwa na mashindano makubwa katika swala hili hasa katika mawazo yangu. Kwa mfano, kuna wakati nilikuwa naenda kuzungumza katika mkutano wa makapera huko Keystone (Colorado), hapa Marekani, na nikapatwa na wazo kwamba, “Mimi ninahitaji kwamba niwe nimepunguza uzito wangu ikifikia wakati wa mkutano huo.” Nikajaribu kufikia lengo hilo lakini kamwe sikufaulu. Ndiposa mawazo mengine yakanijia, “Jumatatu ijayo nitaanza juhudi hizo za kupunguza uzito wangu.” Na wakati mkutano huo ulipokaribia kabisa, pengine wiki mbili kabla ya kuanza, nilikuwa ningali nataka kupunguza kama ratili 10 hivi. Lakini juhudi zangu zote hazikufua dafu. Ndiposa nikamwambia rafiki yangu mmoja wa karibu kwamba, “Wajua nini Kay, mimi ninajisikia kufa moyo sana kwa sababu ya uzito wangu. Kwa kweli siendelei vizuri katika jambo hili. Ningependa kupunguza ratili kumi hivi kabla ya kwenda huko Keystone.” Ndipo hapo nikamwambia uzito wangu ulikuwa ratili ngapi. Naye akaniangalia na kuniuliza, “Ney, wadhani watu hao watakupenda zaidi katika mkutano huo ikiwa utakuwa umepunguza uzito wako?” Jambo hilo liliniguza sana. Ndipo nikamjibu, “Wajua nini Kay, nafikiri kuna kitu fulani katika ubongo wangu kinachofikiria hivyo.” Naye akaniangalia tena na kusema, “Ney, wajua mimi ninakupenda jinsi ulivyo tu. Kamwe mimi sijali kuhusu uzito wa mwili wako hata kidogo.” Hapo ndipo nikaanza kulia. Rafiki wangu Kay alinionyesha neema kubwa siku hiyo wakati ambapo nilinyenyekea mbele zake na kumwambia ukweli wangu. Na wajua nini? Hapo hapo nilipata motisha mpya wa kutoka ndani mwangu ulioniwezesha kupunguza ratili kadhaa za uzito wangu.

Kile ambacho sheria haingeweza kutimiza neema ilifaulu kufanya hivyo. Waebrania 13:9 inasema, “Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu .” Naye Mungu atatenda hivyo kwetu, ikiwa tutakuja kwake tukiwa wakweli.

Tazama Luka 18:9-14 ambapo Yesu alitoa mfano ufuatao: “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtozaushuru. Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: ‘Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtozaushuru. Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.’ Lakini yule mtozaushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: ‘Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.’ Nawaambieni, huyu mtozaushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa”

Njoo kwa Ukweli na Imani

Tukikosa kunyenyekea na kupokea neema yake Mungu hatuwezi kuwa na uhusiano na Yeye. Lakini tunapokuja kwa Bwana na kumwambia vile ambavyo tumeshindwa kufikia viwango vyake vya ukamilifu katika sehemu fulani maishani mwetu Yeye atakutana na hitaji letu kwa njia ya neema yake. Mungu hataki tujaribu kujibadilisha sisi wenyewe. Badala yake, Yeye anataka tuje kwake kwa ukweli na imani, huku tukimletea matatizo yetu yote (1 Petro 5:5-7).

Watu ambao wako na afya nzuri ya kiroho ni wale ambao wanajua sehemu hizo za maisha yao ambazo hazifikii ukamilifu unaotarajiwa na Mungu, na badala ya wao kujiondolea lawama, wanakuwa tayari kusema kwamba, “Bwana nihurumie, mimi ni mwenye dhambi.”

Mafarisayo walifanya juu chini ili kuwa watakatifu, wakajaribu kufuata sheria, lakini shauku kubwa lao lilikuwa kupata sifa kutoka kwa watu. Ndiposa Yesu akawaita, “Makaburi yaliyopakwa chokaa.” Kwa nje wao walionekana kufaa, lakini ndani wao walikuwa watu wenye mioyo iliyokuwa imejaa machungu mengi dhidi yake Yesu. Kwa mfano, wao walifanya bidii sana kuhakikisha kwamba sheria ya “usifanye kazi katika siku ya Sabato” imefuatwa. Hivi kwamba hata wakati Yesu alimponya mtu katika siku ya Sabato kutokana na huruma zake, wao walimsomea vibaya.

Wakati mwingine inakuwa ni rahisi sisi kuwa na uhusiano na sheria, kuliko kuwa na uhusiano na Bwana. Na Shetani angependa sisi kufikiria zaidi kuhusu sheria (amri zake Mungu), badala ya kuweka mawazo yetu kwa Bwana wetu.

Je, sisi tunataka kupata neema yake Mungu. Basi tunahitaji kufika kwake kwa ukweli na unyenyekevu. Yakobo 4:6 inasema, “Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu.”

Miaka kadhaa iliyopita msichana mmoja kijana alikuja kwangu hapo baada ya kikao cha semina ambayo nilikuwa nafanya. Uso wake ulijaa giza, na alionekana kama kwamba amesumbuka sana kutokana na hukumu ambayo ilimkalia vibaya. Lakini tulipoanza kuzungumza niligundua kwamba Kristo alikuwa tayari maishani mwake, lakini ndani yake pia kulikuwa na tabia ambayo aliionea aibu sana. Yeye alikuwa amejaribu sana kuitawala tabia hiyo lakini alikuwa ameshindwa. Kamwe yeye hangejizuia kufanya jambo hilo. Alikuwa amejaribu hata kufanya viapo ili kukatisha tabia hiyo, lakini kamwe havikumsaidia. Na jambo hilo lilipotendeka mara baada ya nyingine, yeye alijihisi vibaya sana, na kujisikia kuhukumiwa kabisa. Ndiposa mimi nikamweleza kwamba Shetani anapenda sisi kutenda dhambi, na hapo baadaye anatusumbua sana kutokana na dhambi hiyo tuliyotenda, na kutuletea hukumu. Ndipo nikamuuliza kama alishawahi kuleta swala hilo mbele zake Bwana. Naye akasema, “Hapana.” Alikuwa akionea dhambi hiyo aibu kubwa hivi kwamba hakuwahi kufikiri kumletea Bwana jambo hilo.

“Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu”
1 Yohana 4:10

Basi nikamweleza, “Wakati mwingine kama jambo hilo litatendeka, badala ya kujificha na kukaa peke yako, badala ya kujihukumu mwenyewe, nataka utumie dhambi hiyo yako kama kitu cha kukumbusha upendo wake Mungu.” Nikamwambia kwamba jambo hilo likitendeka tena, alihitaji kulikiri na kusema maneno kama yafuatayo, “Bwana ninakushukuru kwa sababu mimi ni wako. Ninakushukuru kwa sababu unanipenda. Damu ya Yesu Kristo yanitakasa kutoka dhambi zote. Mimi naungama dhambi hii yangu, lakini kamwe siwezi kujisaidia kutoifanya kama wewe hautaniwezesha. Bwana, naweka nia yangu; naweka nafsi yangu, katika upande wako na wa neno lako. Naomba kwamba uweze kufanya ndani yangu na kupitia kwangu kwa njia ya Roho wako kile ambacho mimi mwenyewe siwezi kamwe kujifanyia?”

Ndipo nikaomba pamoja naye na kwa pamoja tukamshukuru Mungu kwa ajili ya neema na amani kutoka kwake. Ilikuwa wazi kwamba msichana huyu alitaka kubadili na kutubu dhambi hiyo, na kwa kweli alikuwa ashatubu. Basi baada ya mieza kadhaa nilipokea ujumbe kutoka kwake (tayari nilikuwa nimemwomba kunijulisha alivyokuwa akiendelea). Katika barua yake yeye alinifahamisha kwamba alikuwa amefanya yale nilikuwa nimemwongoza kufanya, na akaendelea kusema hivi, “Ney, mimi nimeshangaa sana jinsi katika miezi hii kadhaa iliyopita kila kitu ambacho kilikuwa kinanisumbua uzito wake sasa umepungua, uzito wake sasa umeenda chini ikilinganishwa na hapo mbeleni.” Mbeleni msichana huyo alikuwa ametekwa nyara kabisa na dhambi, na akawa yuko nje ya neema. Lakini aliponyenyekea mbele zake Mungu na mbele yangu na kuleta dhambi yake kwa mwangaza wa neema yake Mungu, Yeye alikutana naye mahali hapo ambapo alikuwa na haja.

Amini Ndio Uweze Kupokea

Waebrania 4:13 inasema, “Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake yeye ambaye kwake tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.” Nayo Warumi 5:20 inasema, “Pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi.” Neema ya Mungu inaweza kupatikana, lakini ni lazima tuiamini ili tuweze kuipokea. Ni lazima tuamini Neno lake Mungu linalosema kwamba neema ipo, ili tuweze kuipokea. Kuna mtu ambaye ameandika na kusema kwamba kuna sharti moja ambalo hatuwezi kuepuka na ambayo hatuna budi kutimiza ili neema iweze kutubadilisha. Sharti hili ni kwamba ni lazima mtu aamini neema yake Mungu. Ni lazima tujitoe kwake Mungu kwa imani. Na Yeye atatenda yale aliyoahidi.

Nikijua kwamba Mungu ni mwaminifu kabisa, na kwamba upendo wake ni wa kweli kabisa, kwamba wema wake ni wa kweli, na matokeo ya jinsi anavyotujali ni kupata uhai tele. Yeye atatenda kulingana na jinsi ambavyo sifa zake zilivyo. Yeye atatufikia hadi chini kabisa mahali tupo. Neema yake itaweza kutubadilisha. Itaweza kuguza malengo yote na misukumo ya mioyo yetu na kutufanya kuwa viumbe vipya. Na hili ndilo jambo ambalo Mungu amejitolea kufanya. Yeye anasema, “Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu” (Waebrania 8:10). Kwa neema ya Mungu atafanya maishani mwetu kile ambacho sheria ya nje haingeweza kufanya.

2 Wakorintho 3:18 inasema, “Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, tunaona kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.” Kubadilishwa kuwa kama Bwana huwa ni safari. Tunapomwini Mungu na kuamini Neno lake Yeye atabadilisha mioyo na fikra zetu. Lakini tunahitaji kuelewa kwamba mabadiliko hayo hayafanyiki mara moja. Ni safari inayochukua muda.

Mwandisho Lewis Sperry Chaffer aliandika kitabu na kusema mengi kuhusu neema. Amenukuliwa akisema kwamba, “Ushuhuda mkuu wa Neno la Mungu ni kwamba kile sehemu ya wokovu wetu, kila baraka ya neema ya Mungu, kwa wakati na kwa milele, zitategemea kile ambacho sisi wenyewe tunaamini.”

Mungu Hutubadilisha Kupitia kwa Neema Yake

Basi sisi tunapata neema ya Mungu kwa njia gani? Kwa kumwendea Bwana kwa udhaifu wetu, katika hali yetu ya kutokuwa na uwezo, katika dhambi zetu, na katika kushindwa kwetu. Mahali hapo ndipo tunafanya uamuzi wa kuamini upendo wake na uwezo wake wa kutubadilisha, wakati tukipumzika katika neema yake. Matokeo yake ni kwamba sisi tunapata uwezo wa kukua.

2 Petro 3:18 inasema, “Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo.”

Katika hadithi ya Mwana Mpotevu inayopatikana Luka 15, Mwana Mpotevu aliondoka nyumbani, akafuja mali ya babake, lakini mwishowe akatambua haja ya kupata fadhili za baba yake (mstari wa 17). “Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.” Yeye alinyenyekea na kwenda kwa baba yake. Akawa mkweli wakati alipokutana na baba yake. Lakini wajua nini? Kaka yake mkubwa hakupendezwa na jambo hilo hata kidogo. Kwa kumkemea baba yake kwa sababu ya kumwonyesha kijana mdogo neema, kijana huyo mkubwa alikuwa akiwakilisha watu wale ambao hufuata sheria kwa dhati. Kwa sababu msimamo wake ulikuwa kwamba kijana huyo mdogo hakuwa amefuata sheria ya babake, na kwa hivyo hastahili neema ya baba. Lakini baba alimpenda mwanaye (mpotevu) bila kujali kile ambacho yeye alikuwa ametenda.

Uhusiano kati yako na Mungu ni wa nguvu zaidi kuliko sheria. Shauku ya Shetani ni sisi kushikanishwa na sheria ili tutembee hapa na pale huku tukiwa twajisikia kuwa na hatia. Lakini Bwana anatwambia katika Warumi 8:1, “Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo.” Katika neema sisi hupata nguvu zinazozidi zetu binafsi. Tunaye Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye hutwezesha kufanya mapenzi yake. Maisha yanayoongozwa na Roho ni ya kujua neema yake Mungu toka siku moja hadi nyingine. Maisha yaliyojazwa Roho ni yale ya kukiri wakati tunapofanya makosa na kuweza kuyarudisha maisha yetu kwa Mungu muda baada ya mwingine. Ni wakati huo ndipo tunachukua jukumu la kibinafsi kuhusu dhambi zetu, na kumwomba Mungu kutubadilisha ili tuweze kukua.

Hapo Msalabani Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kutokana na uovu wetu wote. Sisi tulikuwa wenye hatia na Yeye alilipa gharama ya hatia zetu. Tendo la kuungama dhambi zetu ni tendo la sisi kushughulikia kile kitu ambacho hakifai maishani mwetu, na kutilia maanani kile ambacho tayari kimelipiwa kwa njia ya msalaba. Sisi hufanyika watu wa Mungu kwa njia ya kuwa wanyenyekevu na wakweli kuhusiana na dhambi zetu na kukubali neema yake Mungu ili tukaweza kukua.

Mwandishi John Powell alisema yafuatayo, “Sisi hudhani kwamba ni lazima tubadilike, tukue na tuwe wazuri ili tuweze kupendwa. Lakini ukweli ni kwamba, sisi tumependwa na tunapokea neema yake Mungu ili tuweze kubadilika, kukua na kuwa watu wazuri.”

Kile ambacho kinaweza kutuzuia kupata uponyaji wote ni kiwango chetu cha kuwa wazi. Ili tuweze kukua ni lazima tujitolee kwa mambo ambayo ni ya kweli. Neema yake Mungu inatupatia uhuru wa kukutana na Mungu, na pia kuweza kukabiliana na ukweli kuhusu sisi wenyewe, kwa kulingana na Neno lake Mungu. Huku tukijua kwamba tunapendwa kabisa na kukubaliwa naye Mungu, Yeye anatuita ili tuje kwake na chote tulicho nacho ili Yeye atusaidie kupata uhuru wake (Yohana 8:32), na pia uhai tele (Yohana 10:10).

Hakuna Hukumu Tena

Mimi ninakumbuka msichana mmoja kijana ambaye alikuja kwangu ili nimpe mawaidha. Kwa maelezo yake mwenyewe, tumbo lake lilijaa ‘maji,’ na hali ya kujihisi kuhukumiwa ilikuwa imemkalia vibaya, na hata hangeweza kulala. Alikuwa katika hali ya kujihukumu kabisa, na moyo wake ulijaa woga na aibu. Sababu ya kujisikia hivyo ilikuwa kwamba alikuwa amejiingiza katika uasherati. Yeye alijua Neno la Mungu linasema kwamba hakustahili kujiingiza kwa mambo kama hayo. Basi akajipata kwamba ametekwa kwenye mtandao wa dhambi, na hangemwambia mtu yeyote jambo hilo, kwa sababu aliogopa kukataliwa na watu. Huku akiwa ameinamisha uso wake, yeye alinihadithia hadithi yote. Hakuacha jambo lolote nje, kwa sababu alihitaji msaada sana. Kwa kweli alijuta dhambi yake sana. Pia alikuwa mwenye toba. Basi akiwa hapo mbele yangu alikiri dhambi yake kwa Bwana, na kupokea msamaha wake, na neema ya Bwana. Baadaye aliniambia kwamba wakati alikuja kwangu alikuwa katika gereza la hisia nzito ndani mwake. Lakini kile alichopata kutoka kwangu haikuwa kukataliwa, bali ilikuwa ni upendo na kukubaliwa.

Miezi kadhaa baadaye nilipokea barua kutoka kwake. Akasema, “Minyororo yangu ilifunguka, milango ya gereza ikafunguka, mzigo mzito ulitoka mabegani mwangu. Nikajihisi huru na hali ya kuwa mtu mpya. Nilipokuwa katika uwepo wako mimi sikufanya lolote lile. Yote yalitegemea kile ambacho wewe ulifanya. Vile ambavyo ulikuwa. Ulinionyesha upendo wa Mungu na kukubalika kwangu na msamaha kutoka kwake.” Ndipo nami nikamwomba aendelee kuwajibika kwangu, na baadaye akaniambia kwamba kuwajibika huko hakukuwa mzigo kwake. Kwamba yeye alijihisi kuwa salama kwa sababu alikuwa akiwajibika kwa mtu ambaye alikuwa amemchukua kwa njia ya neema. Baadaye akaweza kupata msaada zaidi, na hata akafika mahali pa kuweza kujielewa kwa njia ya ndani zaidi. Akasema kwamba sasa neema haikuwa jambo la kithiolojia tu, bali ilikuwa jambo ambalo mwenyewe ashalipata.

Sheria nzuri, takatifu na kamilifu ilikuwa imemwonyesha dhambi yake, kama kwamba ni kupitia kwa kioo. Lakini yeye akaweza kunyenyekea. Akakiri dhambi yake. Akaiambia nafsi yake ukweli, nami pia akaniambia ukweli, hata kumwambia Bwana ukweli. Na kwa kuja kwake yeye aliweza kupokea neema ambayo aliihitaji. Akaleta dhambi yake kwa mwangaza wa Bwana kwa roho ya unyenyekevu, na kweli jambo hilo lilimwezesha kupokea neema yake Mungu ambayo ilimweka huru na akaweza kukua.

Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu
Warumi 8:1

Hebu jifikirie wewe mwenyewe kuhusiana na zile sehemu maishani mwako ambazo ungali wajihisi kuhukumiwa au unaogopa kukataliwa . . . sehemu ambayo wewe unajihisi kwamba haujakamilika. Tunahitaji kuja kwa Mungu kwa unyenyekevu na kwa ukweli ili kumletea sehemu hizo ambazo tunajisikia kwamba hazifikii viwango vyake. Hakuna haja ya kujificha. Hakuna haja ya kudanganya. Hauna haja ya kujihisi kuhukumiwa.

“Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza . . . Mungu alimtuma Mwanae . . . Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho” (Warumi 8:1-4).

“Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu.” Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni” (1 Petro 5:5-7).

“Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote. . . Maana Kristo ndiye aliyekufa . . . Yeye anatuombea! Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? . . . wala kifo, wala uhai; . . . Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.” (Warumi 8:31-39).