Usiache Kupumua

Vile ambavyo tunaweza kudumu karibu na Mungu …

Sikiliza makala hii:

Tunapoanza uhusiano wetu na Kristo, siku za mwanzo mwanzo huwa siku zetu za fungate. Siku hizo tuna furaha kwamba tumerudishiwa uhusiano na ushirika wetu na Mungu. Dhambi zetu zimesamehewa. Na kwa hivyo kila kitu kiko shwari.

Kusema kweli kila kitu ni shwari.

Lakini katika ulimwengu ambao umeshaanguka kusema kwamba kila kitu ni shwari si kusema kwamba kila kitu ni kikamilifu. Muda si muda siku za fungate huisha. Na hapo ndipo sisi hutambua kwamba tumeleta mizigo kadhaa kutoka maisha yetu ya zamani na kuingiza mizigo hiyo katika uhusiano wetu mpya na Kristo.

Kwa kweli sasa Mungu ametupatia moyo mpya, motisha mpya, mwelekeo mpya; lakini mtu wetu wa kale hakutoka ndani yetu tulipokuwa katika siku zetu za fungate. Kumbe yeye alijificha tu kwenye kiegesho cha gari hapo nyumbani mwetu.

Mwandishi C.S. Lewis aliandika na kusema, “Wewe utajua kwamba upepo una nguvu wakati ukijaribu kuenenda dhidi yake.”

Lewis alikuwa akijaribu kusema kwamba mtu hujua nguvu za dhambi wakati ambapo anajaribu kuacha dhambi yake. Ni wakati huo ambapo sisi kama waumini, wakati tukijaribu kutembea na Mungu, ndipo hapo kwa mara ya kwanza tunajipata kwamba kuna mapambano yaliyoko kati yetu na dhambi, mapambano ambayo huandamana na sisi kujihisi kuhukumiwa.

Wakati mimi nilikuwa mchanga katika Ukristo, jambo la kwanza ambalo nilitambua lilihitaji kubadilika ndani yangu lilikuwa ni lugha niliyotumia. Mdomo wangu ulikuwa ukitoa maneno machafu kila wakati. NIsingalisema hata sentensi moja bila kufanya kiapo. Nakumbuka kwamba nilipoenda kwa mara ya kwanza katika ushirika wangu wa kanisa, ushirika wa kujifunza biblia, hapo ndipo nilitambua kwamba hakuna mtu mwingine ambaye alikuwa akitumia maneno ambayo niliyapenda sana. Hapo ndipo nikatambua kwamba nilihitaji kubadilika. Na kusema kweli mimi nilibadilika.

Lakini wakati mwingi watu huamini mambo ambayo sio ya kweli kuhusiana na swala hili. Wao huamini kwamba mtu yeyote anaweza kubadilisha tabia zake na kuondoa zile ambazo haifai. Kwamba kila mtu anaweza kufanya Uamuzi wa Mwaka Mpya wa kubadilisha mambo haya ambayo hayafai. Kwamba anaweza kujizuia ili asiwe wa kuendesha gari lake kwa mwendo wa kasi. Lakini swala la kubadilisha hasira za barabarani, kubadili hasira zako, hali yako ya kutokuwa na subira -- mambo hayo yote hutoka ndani mwetu, mahali pa ndani sana.

Lakini kulingana na jinsi ambavyo tunaendelea kukua katika mambo ya utakatifu ndivyo ambavyo sisi hutambua kwamba hata zaidi ya tabia hizi ambazo huonekana kwa nje, kuna dhambi kubwa sana ambayo imejificha ndani mwetu. Ndipo hapo tunatambua kwamba mambo hayo hatuwezani nayo. Tunatambua kwamba kamwe hatuwezi kujibadilisha sisi wenyewe. Lakini kujua hivyo hakutufanyi kuacha kujaribu tena na tena.

Katika kushughulikia tatizo la dhambi na katika jitihada za kujaribu kuificha dhambi hiyo, sisi zote hutumia mbinu ambazo zinafanana. Mwanzo kabisa sisi hufanya juhudi zaidi. Tunajikaza zaidi ili tushinde dhambi hiyo. Na tunapokosa kufaulu, ndipo tunaanza kujaribu kuweka nguvu nia zetu kwa kufanya viapo na ahadi: “Kamwe sitatenda jambo hili tena. Sitalitenda tena.”

Lakini muda si muda sisi hujipata kwamba tumeanguka tena. Ndipo hapo sasa tunaanza kutoa visingizio na kuanza kukana dhambi hiyo. Mawazo yetu yanakuwa vifuatavyo: “Kusema kweli kirasmi jambo hili sio dhambi, kama halijaandikwa kuwa ni dhambi hii ni kumaanisha sio dhambi.” Au, “Ikiwa ni mtu mwingine amenifanya kutenda dhambi hiyo, basi kamwe hiyo sio dhambi yangu.”

Lakini mawazo kama hayo pia hayatusaidii na ndiposa sasa tunaanza kujichukia. Basi kuna haja gani ya Yesu kufa msalabani ikiwa sisi wenyewe tunajisulubisha? Ndiposa sasa tunaanza kujipiga makonde makali, “Mpumbavu mimi, kwa nini nimefanya jambo hili tena?” Huenda ikawa kwamba wakati kama huo sisi huwa twajihisi kwamba tunaweza kulipia gharama ya dhambi hiyo yetu.

Inapofika wakati kama huo furaha yote na ukakamavu wote wa maisha huwa ushamwondokea Mkristo.

Wakati huo uhusiano wetu na Mungu huwa ni jitihada tu za kushughulikia tatizo la dhambi. Sisi huwa tunapitisha wakati tu kama Wakristo. Lakini katika Yohana 10:10 Yesu alisema kwamba, “Mimi nimekuja mpate kuwa na uhai — uhai kamili.” Kuna uhai kamili ambao unapatikana katika maisha ndani ya Kristo.

Kwa sababu sasa sisi ni waumini, kuungama dhambi zetu ni njia ambayo Mungu ametupatia ili kusuluhisha swala la dhambi zetu. Na ungamo la dhambi huwa ni jambo lililo na sehemu tatu. Ya kwanza ndio huwa ngumu zaidi. Si kwa sababu tendo lenyewe ni ngumu, bali ni kwa sababu hili ni jambo ambalo huwa ngeni kabisa na hali yetu kama wanadamu. Tunalohitaji kufanya tunapotenda dhambi au kushawishika kwamba tumetenda dhambi, ni kutulia kidogo . . . na kukubaliana na Mungu kwamba jambo hilo ambalo tumetenda ni dhambi. Yohana wa Kwanza 1:9 inasema, “Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote.”

Pili, tunahitaji kukubali kwamba kile ambacho Yesu alifanya msalabani kilimaliza kabisa malipo ya dhambi hiyo yetu. Na tatu, tunahitaji kukubali kuachana na dhambi hiyo na kumgeukia Mungu, jambo ambalo linajulikana kama toba.

Hebu waza kuhuzu mfulululizo wa mambo hayo ambayo wewe ulipitia wakati ulipomkubali Kristo. Ni kwamba ulifika mahali ambapo ulitambua kwamba una tatizo la dhambi. Kwa mfano tuseme mimi nimeenda ziwani kuvua samaki, na mawazo yangu yanaanza kunipeleka huku na huko. Inafika mahali ambapo ninamwona mwanamke mmoja ambaye mavazi yake ya kuogelea yamedhihirisha mwili wake sana. Na ninapoendelea kumtazama ninapata ushawishi kwamba mtazamo huo wangu ni dhambi . . . kwamba nimetenda dhambi ya kutamani. Sasa mimi naweza kuwa na mielekeo tofauti tofauti kuhusiana na jambo hilo. Naweza kutoa visingizio na kusema kwamba, “Kwa kweli mimi ni mwanaume tu. Hakuna lingine ambalo ningaliweza kufanya hapa.”

Au naweza kujiondolea lawama, “Si kwamba mimi nimefanya uzinzi au kitu kingine kama hicho.”

Naweza pia kulaumu wahusika wale wengine, “Kwani mwanamke huyu alikuwa na lengo gani kufika mahali hapa kama amevaa hivyo?”

Lakini pia naweza ungama. Naweza kukubaliana na Mungu kwamba kile ambacho nimetenda ni dhambi. “Bwana Yesu mimi nimetamani . . . moyoni mwangu na akilini mwangu. Naomba msamaha. Nakubali kwamba Kristo alilipia gharama ya dhambi yangu. Bwana, asante kwa kuniondolea adhabu ya dhambi yangu. Mimi nakubali kuachana na dhambi hiyo. Kamwe sitaki kuwa mtu mwenye tamaa. Nataka kuishi maisha safi na matakatifu.”

Huo ndio msururu wa mambo ambayo yanalingana na ungamo la dhambi. Hili ndilo jambo ambalo tunahitaji kufanya kila siku, kila saa, na wakati wowowte ambapo tunajipata tumetenda dhambi.

Tunapoungama dhambi hapo ndipo sisi hutakaswa kutokana na dhambi hiyo. Na uhusiano wetu na Mungu unarudishwa kuwa katika hali bora. Na kwa kweli jambo hilo linapendeza sana, au sivyo? Ni jambo ambalo linafanana na mtu kupunga hewa nzuri ndani mwake kwa nguvu zake zote. Hili ni jambo ambalo linahitaji kupendeza mioyo yetu sana. Lakini pia kuna jambo la mwisho ambalo tunahitaji kushughulika nalo.

Je, twawezaje kujikinga ili tusiwe watu wa kurudia-rudia dhambi mara baada ya nyingine?

Mimi nadhani kwamba sisi kama Wakristo hutambua kwamba tuko na uzima wa milele, na kwamba tumesamehewa dhambi zetu. Lakini wakati mwingi sisi husahau kwamba Roho wa Mungu yuko ndani yetu. Kwa kweli hatukuachwa peke yetu kumfuata Yesu kwa bidii na nguvu zetu.

Shauku la Roho Mtakatifu ni kutuonyesha njia, kutupatia mwongozo na nguvu, na hata motisha. Na katika Waefeso 5:18 Mungu ameamuru, “Mjazwe Roho Mtakatifu.” Safari ya Ukristo huwa ni ya ushirika, sisi tuna wajibu wetu. Wajibu wa Mungu ni kutuonyesha njia, kutuongoza na kutupatia nguvu. Na wajibu wetu huwa ni wa aina mbili. Kwanza tunahitaji kudumu ndani yake Mungu. Neno kudumu ni neno ambalo Yesu alitumia kumaanisha “kujisikia kustarehe ndani yake.”

Kazi yetu ni kujisikia tumestarehe ndani ya Yesu mchana kuchwa. Na hii ni kumaanisha kwamba tuwe watu wa kukaa karibu na yeye siku zote, kwa kiwango chote ambacho kinawezekana.

Hii ni kumaanisha kwamba hatustahili kufanya maombi ya utauwa kwa mara moja tu kwa siku; mbali ni tuombe siku kuchwa; tunapokumbana na jambo lolote tuwe tumpatie Mungu shukrani; huku tukimsifu mchana kutwa wakati wowote tunapowaza kuhusu jambo lolote lile ambalo tunahitaji kumsifu kwa ajili yake. Kumsifu bila kikomo huku tukiungama dhambi zetu wakati wowote ule tunapojihisi kwamba tumetenda dhambi, au kuhakikishiwa dhambi hiyo na Roho Mtakatifu. Tunatoa shukrani kwa Mungu, tunamsifu, na kukiri dhambi zetu na kuomba; mambo hayo ndio ambayo yanatuwezesha kudumu karibu na Mungu siku baada ya nyingine.

Tunadumu ndani yake, na kutokana na hayo Roho Mtakatifu anakuwa huru kutupatia nguvu zake na kutuongoza.

Jambo la pili ni kutegemea. Wewe ushawahi kuona watu ambao wakitembea huku na kule wao huwa wamebeba chupa zilizojaa maji au vikombe vya chai. Siku kuchwa, wakati wowote ule, wanapojihisi kiu tu, wao huwa wanameza tonge ndogo la maji au la chai.

Wao huwa wakitegemea maji/chai/au kahawa hiyo. Wanapojihisi upweke wanameza kidogo. Wanapohisi woga wanameza kidogo. Wanapohitaji kuwaza kuhusu jambo fulani wanameza kidogo. Wakati wowote wanapokuwa na haja, wanapohisi kiu maishani mwao, wao humeza kidogo. Na maana ya mtu kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu ni yeye kuwa na mwelekeo kama huo wa mnywa maji, kumtegemea Mungu kwa kila jambo.

Hii ni kumaanisha kwamba mchana kutwa tunapojihisi hitaji, mwelekeo wetu utakuwa kwamba: “Bwana naomba unipe hekima. Bwana ninahitaji nguvu zako sasa hivi. Bwana sijui nifanye nini sasa. Bwana nipe mwongozo wako.”

Tunapoendelea kumtegemea Mungu na kudumu karibu naye kwa kiwango chote kinachowezekana, Roho wa Mungu anao uwezo wa kutuonyesha njia, kutuongoza, na hata kutupatia nguvu.

Kwa kweli tumesema mengi hapa. Na ningetaka wewe uweze kukumbuka yote ambayo tumesema. Kwa hivyo sasa nitatumia mfano wa mtu anayepumua. Sawasawa? Wakati unapopumua wewe huwa unatoa pumzi nje kutoka mwili wako, halafu tena unavuta pumzi kuingia ndani mwako.

Kutoa na Kuvuta Pumzi

Kutoa pumzi kunafanana na tendo la kuungama. Unatoa hewa mbaya kutoka mwilini mwako. Kumbuka kwamba kuungama ni jambo ambalo linahusisha mambo matatu. Kwanza ni kukubaliana na Mungu kuhusu dhambi yako. Unakubali kwamba Kristo aligharamia malipo ya dhambi. Pia unakubali kuachana na dhambi hiyo kwa njia ya kutubu. Basi unapotoa pumzi nje kutoka ndani mwako wewe huwa unatoa hewa ambayo haifaii ili itoke nje ya mwili wako. Sawasawa?

Tendo la kuvuta pumzi ndani ni kama kutegemea nguvu za Roho Mtakatifu. Hii ni kumaanisha kwamba unamtumaini Roho wa Mungu ili akuonyeshe njia na akwongoze. Unaamini kwamba Mungu atafanya hayo yote. Na kwa sababu Mungu amesema kwamba tunahitaji kujazwa Roho, tunaweza kuamini kwamba Yeye atafanya hivyo.

Basi tunapovuta pumzi sisi huwa tunasema kwamba, “Bwana naomba unijaze, naomba unipe nguvu, naomba unipe mwongozo. Ninaamini kwamba utafanya hayo yote.”

Ndiposa sisi huvuta pumzi iingie ndani mwetu na pia tunatoa nje ile ambayo haifai. Tunaungama dhambi na pia kumtegemea Roho wa Mungu. Na kama ilivyo kweli katika tendo la kupumua, hili silo jambo ambalo utalifanya mara moja tu kwa siku. Hapana. Siku kuchwa utalifanya jambo hilo. Utalifanya mchana kutwa, utoe pumzi nje na pia uivute ndani mwako. Wakati wowote ukifanya dhambi toa pumzi nje (ungama), na pia uvute pumzi ndani (kwa kumtumaini Roho wake Mungu ili afanye kazi maishani mwako).

Mara ya kwanza jambo hili litaonekana kuwa ni kama mzaha, lakini hebu wewe niamini tu, baada ya muda usio mrefu hili litakuwa jambo la kawaida kwako, kama . . . kupumua hewa kulivyo.

Mungu ametuumba ili tuishi maisha mapya. Maisha ambayo yako huru kutokana na nguvu za dhambi na pia ili tuweze kudumu karibu na Mungu.

Hebu tutoe mfano wa mwisho. Hebu chukulia kwamba wewe unapiga mbizi majini huku ukiwa na mtungi wa oksijeni, lakini ambao hauna hewa hata kidogo ndani mwake. Sasa wewe uko ndani ya maji kabisaa, na maisha yako yamekatishwa kutokana na hewa yote ya oksijeni. Hii ndio sababu ni muhimu mtu kutegemea nguvu za Roho Mtakatifu, kwa njia ya yeye kupumua kiroho. Wakati sisi tumetengwa kutokana na Roho Mtakatifu, sisi huwa tumetengwa kutokana na chanzo chote cha nguvu zetu zote za kiroho, nguvu ambazo tunahitaji ili tuweze kuishi maisha ya Kikristo. Wakati kama huo nguvu za dhambi hiyo yetu, na udhaifu wetu unaotokana na uwanadamu wetu, ni mambo ambayo hutulemea sana. Mambo hayo hutulemaza hata tukashindwa kwenda mbele katika maisha yetu ya Ukristo. Lakini tukiwa na nguvu za Roho Mtakatifu, Yeye anao uwezo wa kutuongoza hadi maisha yetu yafikie viwango vipya vya Ukristo ambavyo mbeleni hata hatukujua vipo. Wajibu wetu ni kupumua tu.