Je, Uhusiano Huu Ni Wa Kudumu?

Jinsi tunaweza kujua kwamba uhusiano wetu na Mungu uko salama.

Sikiliza makala hii:

Kuna mahusiano mengi maishani ambayo si ya kudumu. Watu hupeana talaka, marafiki huacha kuwasiliana, wakati mwingine hata kifo huja kwa mtu ambaye tunampenda. Basi pengine wewe unashangaa kama uhusiano huu mpya kati yako na Mungu . . . kwa kweli ni wa kudumu?

Lakini Mungu anatwambia, “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa” (Waebrania 13:5). Tunapoweka imani yetu kwa Yesu, na kumtaka aingie maishani mwetu, tunafanyika wana wake milele na tutaweza kudumu salama katika upendo wake.

Kwa kweli sisi hatukufanyia kazi uhusiano huo wetu na Mungu, na hatuna haja ya kukazana sana ili tuendelee kujishikilia ndani mwake. Biblia inasema wazi kuhusu jambo hili. Wakati tulipoweka imani yetu kwa Yesu Kristo, Mungu mwenyewe alitukubali.

“Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa” (Warumi 3:22-24).

Maandiko yafuatayo yatakusaidia kujua mambo ambayo sasa ni ya kweli kuhusu uhusiano wako na Mungu.

Kabla ya sisi kukubali Ukristo

Pengine wewe hukujua mambo yafuatayo. Lakini kabla ya wewe kufanyika kuwa Mkristo Biblia inasema kwamba tulikuwa:

  • maadui wa Mungu (Warumi 5:10)
  • watu ambao hawawezi kujisaidia (Warumi 5:6)
  • watu wasiomcha Mungu (Warumi 5:6)
  • wenye dhambi (Warumi 5:8)
  • waliopotea (Warumi 18:11)
  • maskini (Ufunuo 3:17)
  • vipofu (2 Wakorintho 4:4)
  • chini ya hukumu yake Mungu (Yohana 3:36)
  • tumekufa dhambini (Waefeso 2:1)
  • wajinga, watumwa wa tamaa za miili yetu (Tito 3:3)
  • tukifanya matendo maovu (Wakolosai 1:21)
  • mbali na Mungu (Waefeso 2:13)
  • bila tumaini (Waefeso 2:12)
  • tukitembea gizani (Yohana 8:12)

Lakini kwa sababu sasa sisi ni Wakristo

Kutoka wakati tunapompokea Kristo maishani mwetu tunakuwa na uhusiano tofauti na Mungu, pia tunapata maisha mapya. Hivi ndivyo ambavyo Biblia inasema kutuhusu, kutokana na Kristo sasa kuwa maishani mwetu; sasa sisi:

  • tuko na amani na Mungu (Warumi 5:1)
  • tu watoto wa Mungu (Yohana 1:12)
  • tumesamehewa kabisa (Wakolosai 1:14)
  • tumeletwa karibu na Mungu (Waefeso 2:13)
  • tumewekwa muhuri wa Roho Mtakatifu (Waefeso 1:13)
  • hatuishi gizani (Waefeso 5:8)
  • tu washirika wa ufalme wake (Wakolosai 1:13,14)
  • twapendwa na Mungu (1 Yohana 4;9,10; Yohana 15:9)
  • tumepewa uhai wa milele (Yohana 3:16)
  • tu salama katika upendo wake Mungu (Warumi 3:38,39)
  • tumeokolewa kwa neema ya Mungu (Waefeso 2:8,9)
  • Kristo anadumu mioyoni mwetu (Waefeso 3:17)
  • tumechaguliwa na Mungu (Waefeso 1:4,5)
  • tumevuka mauti na kuingia kwa uhai (Yohana 5:24)
  • tu hai ndani yake Kristo (Waefeso 2:15)
  • tu wenye haki machoni pake Mungu (2 Wakorintho 5:21)
  • tunachungwa na Mchungaji ambaye anatujali (Yohana 10:27)

Yesu alisema, “. . . kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu” (Yohana 6:37). Huku akielezea jambo hilo zaidi akasema kwamba, “Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. Mimi na Baba, tu mmoja” (Yohana 10:28-30). Tu salama kabisa mikononi mwake.

Zaidi ya hayo tunaweza kusema pamoja na mtume Paulo: “nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6).

Yesu alilipa gharama yote ya dhambi zetu na kama tutampatia shukrani kwa kufanya hivyo, na kumpokea maishani mwetu, huku ndani mwetu tukiwa na shauku ya kufanya maisha yetu kuwa yake, Yeye anatufanya watoto wake na anatupatia msamaha kamili na kukubalika mbele zake.

Uhusiano wetu na Mungu umelindwa

Uhusiano wetu na Mungu umelindwa, sio kutokana na mambo ambayo tutafanya, bali kwa sababu ya sifa zake Mungu, na kutokana na kifo ambacho Yesu alitufia. Yesu alinunua uhusiano wetu naye, akafutilia mbali adhabu ya dhambi zetu ambazo zilisimama kati yetu na Mungu. Hii ndio sababu tunafanyika wana wa Mungu, tunasamehewa, na Mungu anaishi ndani yetu, na pia tunatangazwa wenye haki machoni pake, kwa sababu Yesu hufunika dhambi zetu. Cha kuhuzunisha ni kwamba sisi bado hutenda dhambi. Tungali twajipata tunafanya mambo kwa kufuata maslahi yetu wenyewe, badala ya kutafuta maslahi yake Mungu. Lakini jambo hilo halibadilishi usalama ulioko katika uhusiano wetu na Kristo. Sisi huwa tumesimama salama katika uhusiano huo kutokana na yale ambayo Mungu amesema kuhusu uhusiano huo. “Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 5:1).

Wokovu kupitia kwa Yesu ni kipawa chake Mungu bila shaka, ambacho tunapokea kwa imani. Hapo ndipo tunaanza uhusiano na Mungu ambao utadumu milele. Uhusiano huo wetu na Kristo hautegemei utakatifu wa kibinafsi, kiwango cha imani yetu, kujinyima kwetu, matendo yetu mema, au hata matendo yetu ya kidini. Kusudi la Mungu sio kwamba tujishughulishe na bidii tunazofanya ili kumpendeza. Shauku lake ni kwamba mawazo na mwelekeo wetu uwe kwa Yesu.

Kinyume na mahusiano mengine ya hapa ulimwenguni, uhusiano kati yetu na Mungu uko salama salimini, kwa sababu Yeye ndiye alituleta katika uhusiano huo hapo mwanzo, na Yeye pia ni mwaminifu kutudumisha hata kufikia uzima wa milele. Wakorintho wa Kwanza 1:9 inasema, “Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.”