Imani Hailingani na Hisia Zako

Kuelewa jinsi tunaweza kumwamini Mungu…

Sikiliza makala hii:

Niliweka maji ya limau kwenye bilauri langu, maji baridi kabisa, halafu nikanoa penseli yangu, na kutoa biblia yangu kutoka kwa kibeti, nikiwa na shauku ya kuanza kazi yangu ya ziada niliyopewa na mwalimu. Hapo wakati wa mchana mkufunzi wangu wa kosi ya shule ya Biblia alikuwa ametuagiza, “Mkija darasani tena mniletee ripoti ya yale yote ambayo kitabu cha Warumi kinasema kuhusu imani.” Nami nikaonelea hiyo kazi ni rahisi kabisa, kwamba haingenichukua muda mwingi.

Lakini nikapigwa na butwaa. Punde si punde nikatambua kwamba neno imani limetumika mara nyingi katika kitabu cha Warumi, na kwa hivyo mafunzo yangu yangechukua muda zaidi ya nilivyodhani.

Kutoa maana ya imani

NIlipokuwa nikisoma yale ambayo kitabu cha Warumi kinasema kuhusu imani, nikajipata nikijiuliza swali, Huenda ikawa imani ndio kitu muhimu kabisa maishani mwangu, lakini ninawezaje kutoa maana ya imani? Imani ni nini?

Akili yangu ikakumbuka miaka minane iliyopita, wakati nilijiunga na kikundi cha Kikristo kijulikanacho kama Campus Crusade for Christ (Wenye Kufanya Injili Katika Vyuo Vikuu kwa Ajili ya Kristo). Wakati huo mimi sikuelewa maana ya kutembea kwa imani. Lakini sasa nikajiambia: sasa hivi uelewaji wangu ni wa hali ya juu. Lakini hata kwa kutumia yale yote ambayo nilikuwa nimejifunza kuhusu imani, nilijipata kwamba singeweza kutoa maana ya imani.

Walakini mimi nilijua kwamba Biblia ina maandiko mengi ambayo yanaongea kuhusu imani, kama vile “Mwadilifu kwa imani ataishi” (Warumi 1:17) na “Hivi ndivyo tunavyoushinda ulimwengu: kwa imani yetu” (1 Yohana 5:4). Lakini nikashangaa kutambua kwamba kamwe singeweza kupata maneno rahisi, maneno yangu mimi mwenyewe, ya kueleza maana ya neno imani; kwa kweli sikuweza kujaza pengo hili: “Kwangu imani ni ____________________________.”

Ndiposa nikafanya ombi: Bwana, wewe waweza kusema imani ni nini?

Hapo ndipo hadithi moja ikaja akilini mwangu ambayo Yesu aliambia mtu fulani, “Sijaona mwenye imani kama hii hata katika Israeli.” Ni nini hicho ambacho Yesu aliita “imani kama hii?”

Nikafungua hadithi hiyo katika Luka 7 inayohusu jemadari mmoja ambaye alikuwa radhi kuamini kwamba Yesu angemponya mtumishi wake mwaminifu ambaye aliyempenda sana na ambaye alikuwa karibu kufa. Jemadari huyo akamwambia Yesu, “Sema tu neno, na mtumishi wangu atapona” (Luka 7:7). Halafu jemadari huyo akatumia mfano wake wa kibinafsi kuonyesha kwamba yeye alielewa maana ya neno lake kuchukuliwa kuwa la kweli na anayeambia kutii.

Kwa kumjibu Yesu aligeukia umati ambao ulikuwa ukimfuata na kusema, “Sijaona mwenye imani kama hii hata katika Israeli” (Luka 7:9). Hapa ni kama Yesu anasema “imani kuu” kama hii ni kumchukua tu kulingana neno lake.

Je, maana kama hii inaweza kupatikana mahali kwingine katika Maandiko? Kwa sababu Waebrania 11 huchukuliwa kuwa ndio “ukumbi mkuu wa imani,” hapo basi ndipo nilienda.

Kuchukua Neno la Mungu Kuwa la Kweli

Baada ya kusoma Waebrania 11 mara baada ya nyingine, na kupata Maandiko yote ambayo yako humo ambayo yanatumia maneno “kwa imani,” nilianza kutambua kwamba watu wote ambao wametajwa humo walishiriki jambo moja kwa pamoja: haijalishi mwandishi wa Waebrania alikuwa anamzunguzia nani, kila mmoja wa watu hao alichukua neno la Mungu kuwa la kweli, na akatii amri yake Mungu. Ndiposa watu hao wakakumbukwa katika imani yao.

Kwa mfano, Mungu alimwambia Noa kujenga Safina kwa sababu Yeye angeleta gharika kubwa. Noa akachukua neno la Mungu kuwa la kweli, na kujenga safina (Waebrania 11:7).

Mungu akamwambia Abrahamu aende mahali ambapo angepokea urithi wake. Abrahamu naye akachukua neno la Mungu kuwa la kweli, akaacha mahali alikuwa amezoea, akaondoka na kwenda (Waebrania 11:8).

Tena Mungu akamwonyesha Sara (ambaye alikuwa amepitisha miaka ya kupata watoto) kwamba angepata mimba na kumzaa mwana. Maandiko yanasema: “Aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake” (Waebrania 11:11). Sara akachukua neno la Mungu kuwa la kweli.

Bila kujali hali ambazo zilizokuwepo, bila kujali ubishi na falsafa za kiakili, bila kujali hisia za mhusika, kila ambaye anatajwa katika Waebrania 11 alimwamini Mungu na Neno lake na kuchagua kuwa mtiifu.

Ndipo hapo nikaanza kuwaza: Ikiwa Luka 7 na Waebrania 11 zinaonyesha imani kuu, je, kuna maandiko ambayo yanaonyesha ukosefu wa imani?

Hapo ndipo nilikumbuka tukio ambalo linapatikana katika Marko 4, siku ambapo Yesu alikuwa amekamilisha mahubiri na mafundisho yake ya siku hiyo hapo kwenye ufuo wa ziwa la Galilaya. Ndipo akawaamuru wanafunzi wake kwenda ng’ambo nyingine ya ziwa hilo. Hapo mwanzo wanafunzi wa Yesu waliamini Neno la Yesu na kuingia kwenye mtumbwi pamoja naye, na kuanza safiri kwenda ng’ambo hiyo nyingine. Lakini dhoruba ilipoanza, wao walianza kuogopa na kuanza kupoteza ujasiri wao kwamba wangefika ng’ambo hiyo nyingine. Basi wakati Yesu aliwauliza, “Je, bado hamna imani” (Marko 4:40), kweli Yeye angeweza kutumia maneno yafuatayo: “Mbona hamchukui Neno langu kuwa la kweli?”

Daima mimi ninapendezwa na mstari wa kwanza wa Marko 5: “Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng’ambo ya ziwa.” Neno la Yesu likawa la kweli.

Kupitia uchunguzi wangu wangu wa maandiko hayo matatu yaliyoko hapo juu mimi nimepata maana rahisi na inayofaa ya neno imani: Imani ni kuchukua neno la Mungu kuwa la kweli. Basi kwa kweli mimi sikuwa na uhakika kwamba ningekuwa na ripoti ya mambo yote ambayo yametajwa kwenye kitabu cha Warumi kuhusu imani, lakini nilijua kwa kweli kwamba siku hiyo nilijifunza kitu ambacho kingekuwa na maana kubwa zaidi maishani mwangu hasa katika safari yangu pamoja na Mungu.

Mungu anasema nini kuhusu Neno Lake?

Lakini nilikuwa ningali na swali moja. Kama imani ni kuchukua neno la Mungu kuwa la kweli, Mungu anasema nini kuhusu neno lake? Jibu lenyewe nililipata katika Maandiko:

“Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe” (Mathayo 24:35).

“Majani hukauka na ua lake huanguka; bali Neno la Bwana hudumu hata milele” (1 Petro 1:24-25).

Maandiko haya yalikuwa yakiniambia kwamba kila kitu maishani kinaweza kubadilika, lakini Neno la Mungu halibadiliki. Ukweli wake haubadiliki. Nilikuwa nimeanza kuona jinsi ambavyo imani yangu katika ahadi zake Mungu ingeweza kuniathiri katika maisha yangu yote ya baadaye.

Kwa mfano, mimi huwa na hisia za nguvu sana. Wakati mwingine mimi huwa na furaha isiyo kifani, na wakati kama huo mimi hufikiri kwamba sitawahi kuwa na huzuni tena. Lakini mara nyingine ninapatwa na huzuni kubwa, hivi kwamba najihisi sitawahi kuwa na furaha tena . . . ilhali wakati mwingine mimi huwa sijihisi kitu chochote kile.

Lakini hata ingawa mimi huwa na hisia za nguvu hivyo ambazo hubadilika-badilika, Neno la Mungu

  • ni la kweli kushinda hisia zote ambazo mimi huhisi
  • ni la kweli kushinda ujuzi wowote ule ambao naweza kupitia
  • ni la kweli kushinda hali zozote zile ambazo ninaweza kuwa nazo
  • ni la kweli kushinda kitu kingine chote ulimwenguni.

Kwa nini? Kwa sababu mbingu na nchi zitapita, lakini Neno la Mungu halitapita. Hii ni kumaanisha kwamba haijalishi vile ambavyo najihisi au ujuzi wote ambao ninaweza kuwa nao, daima naweza kutegemea Neno lake Mungu kama ukweli halisi ambao kamwe haubadiliki maishani mwangu.

Basi mawazo yangu yakarudi na kukumbuka jioni hiyo ambayo nilikuwa ninafanya kazi yangu ya ziada kama siku ambayo ilibadilisha maisha yangu kabisa. Mara nyingi baada ya siku hiyo, wakati hali zilizonizunguka pamoja na hisia zangu zilipoonekana kuwa ni za kweli zaidi, hapo ndipo nimechagua kuamini kwamba Neno la Mungu ni la kweli zaidi kushinda kitu kingine kile. Nimeamua kutembea kwa imani.

Lakini wakati mwingine uchaguzi huo wa kufuata imani umekuwa mgumu.

Na hisia je?

Lakini kuna siku ambapo hata baada ya ufunuo huo wa siku hiyo ya kazi ya ziada sikuweza kuhisi upendo wake Mungu. Basi wakati kama huo ilinibidi kufanya uchaguzi wa aidha kuweka mawazo yangu kwa hisia hizo za kwamba sihisi kupendwa na Mungu, na kuziruhusu zinipeleka katika hali ya kujihurumia, au kusema kwamba, “Bwana, mimi sijihisi kupendwa nawe. Huo ndio ukweli wa mambo. Hapo ndipo nilipo sasa. Lakini Bwana, Neno lako linasema kwamba unanipenda. Kwa hakika wewe umesema kwamba unanipenda kwa upendo wa milele (Yeremia 31:3). Kamwe hukomi kunipenda. Upendo wangu kwangu utaendelea kudumu hata wakati mambo mengine yote yanashindwa (1 Wakorintho 13). Neno lako linasema kwamba wewe hauna mapendeleo. Hii ni kumaanisha kwamba ulimwenguni kote hakuna mtu ambaye unapenda kuniliko. Basi Bwana ninakushukuru kwa sababu unanipenda (Matendo 10:34). Neno lako ni la kweli kushinda jinsi ambavyo mimi ninajihisi.”

Ndipo hapo nikaanza kutambua kwamba wakati ambapo nimeshughulikia hisia zangu kwa njia hiyo, jambo hilo lilinipatia uhuru wa kuwa mkweli kwa Mungu, na pia kuwa mkweli kwa hisia zangu, na nikaweza kuchagua kuamini Neno lake Mungu, wakati ambapo hisia zangu zimekuwa kinyume kabisa na ahadi zake.

Kwa kweli mimi wakati mwingine nimehisi woga, upweke au magandamizo ya kiakili. Moyo wangu ukauma sana kuhusu hali zinazonikumba maishani, na ni wakati kama huo ndipo nimehisi kujaribiwa kuacha kuamini ukweli wa Neno lake Mungu. Lakini mimi nimechagua kuamini Neno lake Mungu kwa kutumia nia yangu. Mara elfu baada ya nyingine mimi nimekuwa nikifanya ombi lifuatalo, “Bwana mimi ninajihisi hivi . . . lakini Neno lako linasema . . .”

Na ujuzi wangu ni kwamba, Mungu hulainisha hisia zangu na kuzilinganisha na Neno lake, kwa wakati wake, na kwa njia zake.

Tumeumbwa viumbe vyenye hisia

Wakati ambapo nimejaribiwa kujihukumu kwa sababu ya hisia zangu, jambo linalonisaidia ni kukumbuka kwamba Mungu alituumba kwa mfano wake, na sehemu moja ya mfano wake ni kwamba sisi ni viumbe vyenye hisia. Hisia sio dhambi. Hata Kristo mwenyewe alikuwa na hisia. Yeye hakujaribu kuwa katika hali ya “kutohisi.” Kwa kweli Yeye hakuficha hisia zake; badala yake Yeye aliingiza hisia zake katika uhusiano wake na Baba yake. Alikuwa mtu mwaminifu, mkweli, asiye na hadaa. Hapo katika Bustani ya Gethisemane, katika usiku ule kabla ya Yesu kusulubiwa, Maandiko yanatwambia kwamba Yeye “alisumbuka sana,” “akawa na majonzi mengi,” “akawa na machungu mengi,” “akaugua” (Mathayo 26:37-38; Marko 14:33; Luka 22:44).

Kwa kweli hata sisi tuna uhuru mkubwa wa kuwa wakweli kwa Bwana kuhusiana na hisia zetu, kumwambia mahali ambapo sasa tupo kwa ukweli wote, na kile ambacho kinaendelea maishani mwetu.

Je, witikio wetu ni upi?

Biblia imetwahidi kwamba sisi ambao tunampenda Mungu kwa ukweli, matokeo ya kile jambo linalotendeka maishani mwetu ni sisi kuundwa kwa mfano wake Kristo (Warumi 8:28-29). Wengi wetu tumefanya maombi haya: “Bwana, naomba unifanye niwe zaidi kama wewe. Naomba unifananishe na mfano wa Kristo.” Lakini kila ambacho tunataka ni Mungu atupatie dawa ya kututuliza, ili tuwe hatuna fahamu wakati Yeye anafanya upasuaji wa mioyo yetu kwa ajili ya kutufananisha na sifa kamili ya Kristo. Kamwe hatutaki kuamka hadi wakati ule mabadiliko hayo yatakamilika! Tunataka matokeo yake bila kupitia uchungu wake.

Lakini Mungu hafanyi kazi hivyo. Bwana hujali mambo ambayo tunapitia maishani, lakini mimi naamini kwamba Yeye ana haja zaidi ya jinsi tutapokea mambo hayo. Jinsi tutakavyopokea yanayotendeka maishani mwetu hutegemea nia zetu. Yeye huruhusu majaribu na masumbuko kuingia maishani mwetu ili sisi tupate nafasi ya aidha kuamini hisia zetu na ujuzi wetu wa maisha, au tuweze kuchukua neno lake kuwa la kweli.

Mimi nimejifunza kuwa na mazoea ya kuchukua Neno la Mungu kuwa la kweli—na sasa imekuwa moja ya tabia zangu! Wewe na mimi tunaweza aidha kuchagua kusikiliza hisia zetu, mawazo yetu, au hali zinazotukumba kutuongoza, au tunaweza kukuza tabia ya kuchukua neno la Mungu kuwa la kweli; hata wakati ambapo hisia zetu na ujuzi wetu maishani unatwambia mambo tofauti. Kupitia nia zetu tunahitaji kufanya uchaguzi wa kuamini kwamba Neno la Mungu ni la kweli hata kushinda hisia tunazohisi.

Mimi nimejitolea kabisa maishani mwangu kutegemea Neno lake Mungu, na Mungu naye amenibariki katika kujitolea huko kwangu. Lakini kuna wakati mimi nimejaribiwa kuacha kujitoa hivyo, kwa sababu wakati kama huo ilikuwa vigumu kuamini kwamba kuna kitu ambacho ni kweli zaidi ya mambo ambayo nilikuwa nikipitia. Wakati huo hisia zangu zilikuwa zajihisi tofauti kabisa na mwongozo wa Neno lake Mungu. Lakini mara baada ya nyingine, mimi nimetambua kwamba Mungu ni mwaminifu kwa Neno lake.

Makala haya yametolewa kutoka kwa kitabu cha Ney Bailey Faith Is Not A Feeling (Imani Hailingani na Hisia Zako). Haki ya Kunakili © 2002. Kilichochapishwa na WaterBook Press. Makala haya yametumika kwa kibali cha mwandishi.