Hali Halisi ya Imani

Sikiliza makala hii:

Kila siku sisi hufanyisha imani kazi. Asilimia tisini na tisa ya kila kitu ambacho tunaamini au kutilia maanani maishani mwetu huwa kinatokana na imani. Imani ni jambo la kimsingi katika maisha yote. Kwa mfano, hebu tuseme kwamba wewe ni mgonjwa. Unaenda kwa daktari ambaye hata jina lake huwezi kutamka vizuri, na ambaye hata hujadhibitisha shahada zake. Yeye anakwandikia kijikaratasi cha dawa kwa maandishi ambayo huwezi kusoma. Ndipo hapo unafululiza hadi kwa duka ambalo wanauza dawa na unauziwa dawa na mtu ambaye humjui kibinafsi, ambaye anakupatia vijidawa ambavyo wewe huwezi kuelewa jinsi vilivyotengenezwa. Halafu unafika kwako na kunywa dawa hizo kulingana na maagizo ya muuzaji huyo wa dawa. Wakati huu wote ukiwa na imani timamu. Kwa kweli imani pia ni msingi wa maisha ya Kikristo. Neno hilo limetumika mara 232 katika Biblia yote.

Imani Ni Nini

Kwanza ni muhimu sisi kusema kile ambacho imani sio.

  • Imani sio hisia, maanake imani sio kuhisi vizuri kuhusu Mungu.
  • Imani sio kuruka na kujiingiza mahali ambako mna giza bila kufikiria, hata bila kuwaza kuhusu ukweli wa mambo ulivyo.
  • Imani sio nguvu za kilimwengu ambazo hukwezesha kupata yale ambayo unataka maishani.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, mawazo kama hayo kuhusu imani hufundishwa katika baadhi ya makanisa yetu.

Katika kitabu chake Christianity in Crisis (Ukristo Ukiwa Taabani) mwandishi Hank Hanegraff anahadithia kuhusu Larry na Lucky Parker, ambao walimnyima insulini kijana wao ambaye alikuwa akiungua ugonjwa wa kisukari, kwa sababu waliambiwa kile walihitaji tu ni imani (na kwamba wakitumia hizo nguvu) kijana wao angepona. Matokeo yake ni kwamba kijana huyo alizimia kutokana na kisukari hicho na kuaga dunia. Na badala ya wazazi hao kufanya mazishi wao walifanya ibada ya ufufuo huku wakiamini kwamba walikuwa na imani tosha kumfufua mradi waseme maneno yanafaa na kuamini kwa njia ya nguvu kabisa bila kuonyesha kutoamini hata kidogo. Wakaamini wakifanya hivyo nguvu za imani zingemtoa mtoto wao kutoka kwa wafu. Larry na Lucky Parker baadaye walifanyiwa kesi ya kusababisha kifo bila kukusudia, na ya kosa la kumfanyia mtoto mabaya. Kwa nini? Kwa sababu walikuwa na wazo ambalo halikufaa kuhusu imani.

Katika Agano Jipya kwenye vitabu vya injili (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) inaonekana kwamba hata wanafunzi wa Yesu walichanganyikiwa sana kuhusiana na swala la imani. Lakini wao walikuwa na busara tosha ya kumuuliza Yesu kuhusiana na jambo hili. Katika Luka 17 tunaona wanafunzi wa Yesu wakimwomba Bwana aongeze imani yao. Na haya ndiyo yalikuwa majibu yake:

“Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: ‘Ng’oka ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.” Jibu la Yesu ni la kushangaza. Tazama kwamba Yeye hakusema baadhi ya mambo ambayo tumezoea kuambiwa kanisani. Yesu hakuwaambia, “Mnahitaji kufanya bidii zaidi ya kuwa na imani.” Pia Yeye hakusema, “Aminini tu!” Jibu la Yesu lilidhihirisha ukweli muhimu kuhusu hali halisi ya imani. Mbegu ya haradali ndio mbegu ndogo kabisa. Yesu alitumia ukweli huo kufafanua kwamba kilicho muhimu sio kiwango cha imani yetu. Bali kwamba . . . nguvu za imani hutegemea uaminifu wa kile ambacho tunategemea, na sio uhakika wetu kuhusu mambo hayo.

Hebu nifafanue maana ya ninayosema. Hebu tuseme kwamba nimesimama ufuoni mwa ziwa wakati wa wiki za kwanza za msimu wa baridi katika Kusini mashariki mwa Marekani. Ziwa hilo limetanda barafu nyembamba laini. Lakini huku nikiwa na imani na uhakika wa mambo, nimechukua hatua ya kwanza ya kutembea katika barafu hiyo nyembamba ambayo imeumbika muda kidogo uliopita. Lakini hata ingawa nina uhakika sana na “imani kubwa” matokeo ya jambo hilo yatakuwa kupatwa na mshtuko wa baridi kali na mimi kulowa maji kabisa. Mradi tu barafu hiyo ni nyembamba, kiwango changu cha imani hakijalishi. Barafu hiyo haiwezi kutegemewa.

Lakini hebu tuseme sasa ni miezi kadhaa baadaye, wakati ambapo msimu wa baridi umekita mizizi. Nikiwa hapo ufuoni sasa ninaweza kuona kwamba barafu imepata kina cha futi kadhaa. Lakini kwa sababu ya ujuzi wangu wa hapo mbeleni, mimi natahadhari sana ninapowaza kuhusu kutembea katika barafu hiyo. Sina uhakika kwamba barafu hiyo itanishikilia. Kwa sababu niliamini hapo mwanzo lakini haikunishikilia. Basi, hata ingawa sasa nina woga na imani “kidogo sana” kuliko hapo mwanzo, najaribu kutembea humo na kuchukua hatua ya kwanza kidogo ambayo imejaa wasiwasi lakini sasa napata matokeo mazuri ya kuweza kusimama wima katika barafu hiyo. Tofauti ni nini? Tofauti ni katika hali ya barafu yenyewe.

Ni kweli kabisa kwamba nguvu za imani zinategemea uamanifu wa kile ambacho kinategemewa. Lakini…

Kiwango cha imani ambacho mtu huwa kwa kile kinachotegemewa hulingana na ufahamu wa mtu huyo kuhusu kinachotegemewa.

Kwa mfano, hebu tafakari kuhusu mtu ambaye anaogopa usafiri wa ndege. Anapofika katika kiwanja cha ndege kwa mara ya kwanza yeye ananunua bima ya usafiri kutoka kwa moja ya mashine za kununua bima ambazo hupatikana humo. Tena anafunga mshipi wake wa usalama dakika ishirini kabla ya ndege kuambaa hewani, na kusikiliza kwa makini miongozo ya kawaida ikitolewa kuhusu jinsi ya kukabiliana na “hali ya hatari” huko angani. Lakini yeye kamwe hana imani na uwezo wa ndege hiyo kumfikisha mahali anakoenda. Lakini kulingana na jinsi ambavyo safari hiyo inaendelea ndivyo ambavyo abiria huyo huanza kubadilisha tabia zake. Kwanza anafungua mshipi wake, halafu anakula chakula chake cha mchana, na muda si muda anaanza kuongea na abiria mwenzake na hata kufanyiana vichekesho. Mabadiliko hayo basi yametoka wapi? Ni nini kimetendeka? Je, huenda kuna imani kubwa zaidi mtu anapofika futi elfu 36,000 juu? La hasha. Lakini, kulingana na jinsi ambavyo mtu huyo anajifunza kuhusu chombo hicho cha usafiri (ndege) ndivyo ambavyo yeye huendelea kuwa na imani na chombo chenyewe.

Hivyo ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya Kikristo. Jinsi ambavyo tunazidi kumjua Bwana, ndivyo ambavyo imani yetu kwake huongezeka. Hebu basi jifunze kuishi kulingana na ukweli wa Neno la Mungu, badala ya kuishi kulingana na hisia zako. Tumia wakati wako katika Biblia huku ukiwa makini, ukimwomba Mungu aendelee kukufahamisha jinsi Yeye alivyo. Na kweli kuna mahali kwingi ambako unaweza kuanza masomo hayo. Zaburi 145, 146 na 147 ni milango ya ajabu ya Biblia ambayo huonyesha Mungu ni nani. Na unaposoma Biblia mwombe Mungu akufundishe zaidi kuhusu Yeye binafsi, huku ukiwa makini kujua kile ambacho angetaka uamini. Katika hali yoyote ile ambayo unapitia, hebu mwombe Mungu, “Ni jambo gani kuhusu wewe ambalo litakuwa msaada kwangu kujua, wakati ambapo ninaendelea kukutumaini katika hali hii inayonikumba?” Hebu basi fika kwenye Biblia na uwe mwanafunzi wa kusoma kuhusu Mungu na uhusiano wako na wewe.

Wakati mmoja mwinjilisti D.L. Moody alisikika akisema, “Kila siku nilikuwa namwomba Bwana kunipatia imani. Halafu siku moja nikasoma Warumi 10:17 ambapo inasema ‘imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo.’ Ndiposa nikaanza kusoma Biblia yangu, na tangu wakati huo imani yangu imekuwa inakua.