Funzo: Je, tulipataje uhusiano huu na Mungu?

Anza na ombi: “Mungu wangu, mimi nakuomba unene nami kupitia kwa Neno lako. Nena na moyo wangu ili niweze kuelewa kile ambacho unataka kuniambia. Amina.”

Mistari ifuatayo ya Biblia itakusaidia wewe kuelewa kile ambacho Mungu anasema kuwa ni cha kweli kuhusu uhusiano wako na Yeye. Baada ya kusoma kila andiko, swali ambalo linafuata litakusaidia kutambua hasa kile ambacho mstari wenyewe unasema.

(Maandiko yenye herufi ndogo ambayo yako mbele ya kila sentensi ni ya kumwezesha msomaji kutambua “mistari” tofauti tofauti ya Biblia; nambari za mistari ya Biblia iliwekwa ndani ya Biblia zamani za kale ili kusaidia Wakristo kutambua mistari tofauti ya Biblia).

Yohana 1
12 Lakini wale waliompokea (Yesu), wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.

S – Mtu anafanyikaje kuwa mtoto wa Mungu?
(Unaweza kuandika jibu lako hapa chini na uchapishe somo hili ukishamaliza kulipitia . . .)

Unaweza kudhani kwamba wewe mwenyewe ndiye ulichagua kumwamini Yesu, kama vile mtu huchagua kununua gari la aina moja au nyingine, au kuamua atampigia nani kura. Lakini mistari ifuatayo inaonyesha kwamba Mungu alihusika katika swala la wewe kufanyika kuwa Mkristo.

Yohana 15
16 Nyinyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni . . .

1 Wakorintho 1
9 Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.

Waefeso 1
4 Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, 5 Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia.

S – Katika mstari wa 5, lengo la Mungu la kutuchagua lilikuwa lipi?

Waefeso 2
4 Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, 5 hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu nyinyi mmeokolewa.

Wakolosai 1
13 Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. 14 Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.

S – Unapotazama mistari hii, ni mambo gani manne ambayo Mungu amekufanyia?

Warumi 5
9 Kwa kuwa sasa tumefanywa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu.

S – Biblia inaposema kwamba Yesu alituokoa, Yeye alituokoa kutokana na nini?

Waefeso 2
8 Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. 9 Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.

S – Je, sisi ndio hufanyia kazi wokovu wetu?

S – Je, mtu anaweza kupata wokovu kwa kufanya matendo mema?

Tamati ya mambo: Toa muhstasari wa mambo yale ambayo mistari hii imesema kuhusu kushiriki kwa Mungu ili wewe ufanyike kuwa Mkristo:

Sasa unaweza kuchapisha somo hili kwa kubonyeza sehemu ya kulia kwenye ukurasa huu, na kuchagua mahali kulikoandikwa “chapisha.”

Utakapoondoka kwenye ukurasa huu majibu yako hayatahifadhiwa katika ukurasa huu.